Ulinzi waimarishwa hosteli za SAUT Mwanza

MWANZA: JESHI la Polisi Mkoa wa Mwanza limeimarisha ulinzi kwa kuongeza doria na vikundi vya ulinzi Shirikishi katika Kata ya Luchelele Wilaya ya Nyamagana ,zinapopatika baadhi ya hosteli za Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT).

Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Wilbroad Mutafungwa  katika eneo la Mtaa wa Kisoko Kata ya Luchelele wakati wa kikao na uongozi wa wanafunzi wa  SAUT, wamiliki wa hosteli, viongozi wa serikali za mitaa na wananchi wa kata hiyo.

Akizungumza na viongozi hao pamoja na wananchi Kamanda Mutafungwa ameonesha kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na wamiliki wa hosteli wanazoishi wanafunzi kwa kufunga CCTV Kamera kwenye nyumba zao na kuongeza ulinzi kwa kuajiri walinzi wa kampuni binafsi za Ulinzi ili kuzuia na kukabiliana na vitendo vya uhalifu.

“Ninawapongeza kwa kutuelewa pia ninawapongeza askari waliofanya kazi kubwa ya kuimarisha ulinzi, lengo letu ni kukomesha vitendo vyote vya uhalifu.

” Alisema

Kwa upande wake, Padre Japhet Haule, mlezi wa wanafunzi katika Chuo cha SAUT amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kazi kubwa na nzuri ya kudhibiti uhalifu eneo hilo ambapo pia ameomba kuwekwa matuta katika barabara zinazozunguka chuo hicho ili kudhibiti mwendo kasi wa bodaboda kwani wanahatarisha maisha yao na watumiaji wengine wa barabara.

Hata hivyo, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza , Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Sundy Ibrahim amewahakikishia wananchi hao kumaliza kabisa kero ya usafiri eneo hilo na kwenda kukaa na watu wa TANROAD na kushauriana kuona namna ya kufanya ili kudhibiti mwendo kasi wa bodaboda eneo hilo huku Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Mrakibu wa Polisi (SP),Virginia Sodoka akimesema kuwa suala la ulinzi na usalama halina siasa hivyo ametoa onyo na kuwataka wamiliki wa hosteli ambao hawajaweka CCTV kamera kuweka  ili kuimarisha ulinzi.

Habari Zifananazo

Back to top button