Umeme maporomoko Rusumo wafikia asilimia 99.9

MWANZA: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa maporomoko ya umeme wa Rusumo wa megawati 80 unaotekelezwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi umefikia asilimia 99.9 na nchi hizo tayari zimeanza kupata umeme kutoka kwenye mradi huo.

 

Dk Biteko amesema hayo leo Disemba 18, 2023 jijini Mwanza wakati akiongoza kikao cha ngazi ya Mawaziri wa Nishati ambaye yeye ni Mwenyekiti wa Mawaziri wa wanaosimamia mradi huo kutoka nchi hizo tatu za Tanzania, Rwanda na Burundi.

“Tumeridhishwa na maendeleo mazuri ya mradi mpaka sasa, tunawapongeza Bodi na Watendaji kutoka kampuni ya umeme ya Rusumo na wakandarasi kwa usimamizi na utekelezaji wa mradi huu,” amesema Dk Biteko

 

Aidha, Dk Biteko amesema  Mawaziri hao wamekubaliana kuwa, mradi huo uzinduliwe mwezi Machi, 2024 hivyo wamemtaka mkandarasi kukamilisha  mradi huo mapema na atoe cheti cha kukamilisha mradi. Amesema uzinduzi huo utafanyika katika eneo la mradi huku mwenyeji wa shughuli hiyo akiwa ni Tanzania.

Pia, amesema kuwa, mradi huo una umuhimu kwa nchi zote tatu kwani bado nchi hizo zina changamoto ya upatikanaji wa uhakika wa umeme hivyo kukamilika kwa mradi huo kutapunguza changamoto hizo na kuongeza uimara kwenye gridi.

 

Vilevile, Dk Biteko ameshukuru wadau mbalimbali waliopelekea  mradi huo kutekelezwa ikiwemo Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na amewakaribisha kuwekeza kwenye miradi mingine ya uzalishaji umeme inayotarajiwa kutekelezwa nchini.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mafuta, Nishati na Migodi wa Burundi, Mhandisi Seleman Khamissi ambaye alimwakilisha Waziri wa Wizara hiyo amesema kuwa, nchi zote Tatu zimekubaliana kuwa mradi huo uzinduliwe mwezi Machi na kwamba nchi hiyo itafaidika na megawati 27 zitakazotoka kwenye mradi huo ambao utasaidia kupunguza changamoto za upatikanaji umeme kwenye nchi hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button