BUNGE nchini Ghana limekatiwa umeme na Kampuni Umeme ya Serikali (ECG) kutokana na deni la Cedi 23m ambazo sawa na Sh bilioni 4.6.
Changamoto hiyo ilikatiza mjadala kuhusu hotuba ya Rais iliyolenga hali ya taifa hilo.
‘Video’ ilitolewa na vyombo vya habari vya ndani ilionesha wabunge wakiwa bungeni na mwanga hafifu wakiimba: “Dumsor, dumsor”, ambayo ina maana ya kukatika kwa umeme katika lugha ya Kiakan.
Vyombo vya habari vya ndani viliripoti kwamba baada ya changamoto hiyo jenereta la dharura ilirejesha umeme bungeni hapo. Hata hivyo baadhi ya sehemu za bunge zilibaki bila umeme kwa siku nzima kabla ya kurejeshwa baadaye.
Wabunge na wafanyikazi wa bunge waliokuwa wakitumia lifti walikwama mara baada ya changamoto hiyo kutokea, kituo cha TV3 cha Ghana kiliripoti.
Mkurugenzi wa mawasiliano wa kampuni ya umeme, William Boateng aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa limeamua kukata umeme kwa sababu ya kukataa kwa bunge “kuheshimu notisi za madai ya kulipa”.
Imeelezwa baada ya shida hiyo, umeme ulirejeshwa baadaye baada ya bunge kulipa Cedi 13m na kutoa ahadi ya kumaliza deni lililosalia ndani ya wiki moja, Boateng aliongeza.
Ofisa wa fedha wa bunge, Ebenezer Ahumah Djietror alikanusha kuwa bunge linadaiwa kiasi kilichonukuliwa na kampuni ya hiyo.