Ummy afanya mazungumzo na balozi Marekani

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amekutana na Balozi wa Marekani nchini, Dk Michael Battle ambapo wawili hao wamezungumza mambo mbalimbali ya kuimarisha afya ya wananchi wa Tanzania.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika siku ya leo, Machi 23, 2023 kwenye ofisi za Wizara jijini Dodoma Balozi Battle amesema Marekani itaendelea kushirikiana na kuisaidia Tanzania katika masuala ya afya kupitia kituo chao cha kuzui na kusimamia magonjwa (CDC).

“Kupitia CDC tutaendelea kusaidia kuboresha afya za wananchi kupitia sekta ya afya na kutoa mafunzo kwa watoa huduma za afya ngazi ya jamii pamoja na wataalamu wa maabara katika uchunguzi wa magonjwa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya milipuko,” alisema balozi Battle.

Advertisement

Aidha, Waziri Ummy alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania inafanya inafanya vizuri katika jitihada za kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na Watoto chini ya miaka mitano.

“Bado kuna changamoto ya ubora wa huduma na gharama za matibabu kwa wananchi hivyo Serikali inakuja na Bima ya Afya kwa wote ili kuwaondolea adha ya matibabu wananchi wake,” alisema Waziri Ummy

Aidha, waziri Ummy aliongeza kuwa sekta ya afya bado inachangamoto ya uhaba wa watoa huduma kwa asilimia hamsini na kuwa bado serikali inaendelea kuajiri watumishi kila mwaka.

Pia alisema jitihada za kupambana dhidi ya Malaria na TB bado zinaendelea huku kwa upande wa HIV maendeleo ni mazuri katika kufikia lengo la
95-95-95.