Ummy amshukuru Samia bima ya afya kwa wote

Ummy amshukuru Samia bima ya afya kwa wote

WIZARA ya Afya imemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia pendekezo la kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote.

Waziri wa wizara hiyo, Ummy Mwalimu ameeleza hayo muda mfupi baada ya Rais Samia kutangaza kuwa mkutano wa Bunge mwezi huu utapitisha muswada wa sheria kuanzisha bima hiyo.

“Tunamshukuru Rais @SuluhuSamia na Baraza la Mawaziri kwa kuridhia mapendekezo yetu @wizara_afyatz ya kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote. Ni matarajio yetu kuwa kupitia sheria hii tutawezesha wananchi wengi kuwa na uhakika wa matibabu kabla ya kuugua.” aliandika Ummy kwenye ukurasa wake katika mtandao wa kijamii wa twitter.

Advertisement

Juzi wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA), Rais Samia alisema mkutano wa Bunge unaoanza leo Dodoma utapitisha muswada huo.

“Niwaombe sana tutakapopitisha sheria hii Watanzania tukajiunge na mifuko ya bima. Nawapa uhakika tunajua udhaifu uliopo kwenye mifuko yetu ya bima,” alisema.

Rais alisema anafahamu udhaifu uliopo kwenye mifuko ya bima na hatua zimechukuliwa hivyo utakapoanzishwa utakuwa madhubuti wenye sheria na kanuni zitakazowezesha watu wote watibiwe.

Miezi kadhaa iliyopita Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilieleza kuwa upatikanaji wa huduma za afya kwa wote ni haki ya msingi ya kila mwanadamu, lakini pia ni utekelezaji wa lengo Namba tatu la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Stanslaus Nyongo alieleza kuwa taratibu zimekuwa zikizingatiwa kuhakikisha Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inatungwa kwa kuzingatia maelekezo ya Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2020 yanayolenga kufikia bima ya afya kwa wote kwa kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF).