Ummy ataka hospitali nyingine ziige MOI

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu

Waziri wa Afya  Ummy Mwalimu ametaka taasisi nyingine kuiga mfano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI) wa kuanza kuwapigia wagonjwa simu ili kuwajulia hali.

Waziri Ummy amesema hayo kupitia ukurasa wake wa twitter Julai 20, 2023 akiwapongeza  MOI kwa kuanzisha utaratibu wa kuwapigia simu wagonjwa wao, ili kupata maoni, ushauri, pamoja na kuwajulia hali kuwa ni jambo la mfano na linafaa kuigwa na taasisi zote za kutolea huduma za afya.

Advertisement

“Hongereni Taasisi ya Mifupa (MOI) pasi na shaka MOI chini ya uongozi wa Prof. Abel Makubi inakwenda kuwa nzuri zaidi, serikali kwa upande wetu imefanya mengi kuboresha Huduma za afya na sasa tunajikita katika kuboresha ubora wa huduma za afya nchini,”ameeleza  Ummy.

Amesema Serikali  imeendelea kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya kwa kuanzisha programu ya mabadiliko ya kiutendaji kwa wasimamizi na watoa huduma  katika vituo vya umma vya kutolea huduma.

Waziri Ummy amesema serikali imeboresha huduma za afya kuanzia ujenzi wa miundombinu ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vifaa vya maabara, kuajiri na kusomesha wataalamu kwa lengo la kuboresha huduma za afya nchini.

5 comments

Comments are closed.