Ummy atangaza mlipuko wa kipindupindu Dar

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuna mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu katika Mkoa wa Dar es Salaam ambapo wagonjwa 15 walithibitika kuwa na maambukizi na hadi sasa wagonjwa 13 wamepona huku wawili wakiendelea na matibabu.

Ummy alibainisha kuwa mhisiwa wa kwanza wa ugonjwa huo alitokea katika Kata ya Kivule, Wilaya ya Ilala, Aprili 16, 2023.

Alisema hadi kufikia Aprili 28, 2023 wagonjwa 15 waliotolewa taarifa, wagonjwa 13 walikuwa Wilaya ya Ilala na wagonjwa wawili Wilaya ya Kinondoni.

Advertisement

“Tunamshukuru Mungu kuanzia Aprili 24 hakuna kisa kipya kilichopokelewa na hadi leo wagonjwa 13 ambao wametolewa taarifa kati ya 15 wamepona, wagonjwa wawili wanaendelea na matibabu na hali zao zinaendelea vizuri na hakuna kifo kilichotokea hadi sasa,” alieleza.

Baada ya kutoa taarifa hiyo, Ummy alitoa maagizo kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na uongozi wa mkoa huo kuhakikisha wanatibu maji kwa kutumia dawa ya klorini kwenye vyanzo vyote vya maji na kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.

“Nimemuelekeza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kushirikiana na serikali ya mkoa kufanya ukaguzi wa visima vyote vilivyochimbwa na pili kuhakikisha wanaweka dawa ya klorini kwenye vyanzo vya maji, kuchemsha maji ya kunywa kama huwezi basi tuweke dawa ya klorini,” alisema.

Ummy pia aliwataka wananchi kuchukua tahadhari kwa kuepuka uchafuzi wa vyanzo vya maji, kuepuka chakula kilichopoa au kuandaliwa katika mazingira yasiyosafi na salama, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka. Tahadhari zingine ni kuosha matunda kwa maji safi kabla ya kula.

“Jingine ninachotaka kusisitiza ni utiririshaji wa maji taka kutoka chooni, hili lazima tulisimamie kwa wakati,” alisisitiza. Aliwataka watu ambao watapata dalili za kuharisha na kutapika kuwahi haraka katika vituo vya kutolea huduma za afya ndani ya saa 24.

“Kwa hiyo suala la ugonjwa wa kipindupindu kwa watu wenye dalili ni kuwahi haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa sababu mgonjwa anapoteza maji mengi kwa njia ya kutapika na kuharisha… ndani ya saa 24 anapaswa awe amefika ndani ya vituo vya huduma za afya ndio maana tunamshukuru Mungu hatuna vifo kwa sababu watu wameweza kufika kwa wakati.”

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *