Ummy atoa neno likizo, wanaojifungua Watoto Njiti

DAR ES SALAAM: Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema uamuzi wa serikali kutohesabu likizo ya uzazi kwa watakaojifungua Watoto Njiti utachangia kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kiasi kikubwa.

Ummy ameyasema hayo leo ambapo amesema uamuzi huo pia utachangia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa watoto njiti.

Kupitia mtandao wa X Ummy ameandika “Asante Mhe Rais Dk Samia kwa uamuzi huu mkubwa ambao kwa kiasi kikubwa utachangia kuimarisha upatikanaji wa huduma bora kwa watoto njiti na hivyo kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa kasi kubwa.

Advertisement

“Naamini nchi yetu itaandika rekodi nyingine duniani ya kupunguza vifo vya watoto wachanga kwa asilimia kubwa kama tulivyofanikiwa kupunguza vifo vya wajawazito na vifo vya watoto wa umri chini ya miaka mitano, ninawapongeza Watumishi wa afya, Wadau wetu akiwemo Doris Mollel Foundation walioweka msukumo katika kufanikisha hili,”amesema.

Serikali imetangaza kuwa iwapo mfanyakazi atajifungua Mtoto Njiti, kipindi cha uangalizi maalum hakitohesabiwa kama likizo ya uzazi na kwamba likizo ya uzazi itaanza pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum kadri Madaktari watakavyothibitisha.

Kwa upande wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania (UWT) inayoongozwa na Mwenyekiti wake Mary Chatanda pia imepongeza uamuzi huo wa serikali kuhusu wazazi wa watoto njiti na kutoa rai kwa serikali kuharakisha mchakato wa marekebisho ya sheria ya ajira na uhusiano kazini sura ya 366 ili itumike pia kwa upande wa wanawake wafanyakazi wa sekta binafsi nchini.

Kauli za viongozi hao imekuja ikiwa ni siku moja serikali itangaze  likizo ya Wazazi kwa Wafanyakazi Wanawake wanaojifungua Mtoto/Watoto Njiti, na kuwekwa katika chumba na mashine maalum (incubator) chini ya uangalizi wa Wataalamu na  wajiridhishe kwamba afya ya Mtoto/Watoto imeimarika, kipindi chote cha uangalizi hakitahesabiwa kama likizo.

Utafiti wa Afya ya Mama na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini (Tanzania Health and Demography Survey) uliofanyika mwaka 2022, unaonesha vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kutoka vifo 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015-16 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

Pia, utafiti huo unaonyesha kuendelea kupungua vifo vya watoto walio chini ya miaka mitano kutoka 67 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2015/16 hadi kufikia vifo 43 kwa kila vizazi hai 1,000.