Ummy awaita wadau sekta ya afya

DAR ES SALAAM: Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa rai kwa wadau wa maendeleo kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuwekeza kwenye sekta ya afya nchini huku wakiiga mfano wa Kampuni ya uzalishaji wa Dawa ya Cure Afya ambayo iko mbioni kuanza uzalishaji wa dawa hapa nchini.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo Desemba 20,2023 alipotembelea Kiwanda kipya cha utengenezaji dawa cha Cure Afya ambacho kipo Wilaya ya Kigamboni jiijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuona utayari wa kiwanda hicho kutengeneza dawa kwa ajili ya soko la ndani ya nchi pamoja na nchi jirani.

“Dawa zinazozalishwa zitarahisisha upatikanaji wake kwa wakati, tofauti na tukiagiza dawa nje ya nchi zinachukua miezi 6 hadi 9 kufika hivyo inachukua muda mrefu mpaka kufika nchini”. Amesema Waziri Ummy.

Aidha,Amesema serikali imejizatiti kukuza uzalishaji wa dawa wa ndani ili kupunguza gharama ya uagizaji kwani Tanzania ni miongoni mwa nchi nne za Afrika ambazo zinatambulika kwa umahiri kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na Shirika la Afya Duniani WHO.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Cure Afya, Paresh Ghelani amesema kuwa wako tayari kwa uzalishaji wa dawa kuanzia Januari 2023 ikiwa ni takwa la serikali katika uwekezaji wa viwanda kwa mahitaji ya nchi ambayo yatakwenda kurahisisha upatikanaji wa dawa kwa wakati na gharama nafuu.

Haya ni matokeo chanya ya uhamasishaji fursa za uwekezaji wa viwanda nchini yanayofanywa na serikali chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ya sekta ya afya nchini katika kuendelea kuboresha sekta hiyo na kuifanya Tanzania kuwa kituo cha utalii tiba ukanda wa Afrika Mashariki.

Habari Zifananazo

Back to top button