Ummy: Magonjwa ya akili yaingizwe bima ya afya

WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu amesema umefika wakati magonjwa ya afya ya akili yaingizwe katika mfumo wa bima ya afya ili wananchi wapate msaada wa kisaikolojia na matibabu.

Katika Kongamano la Kwanza la Afya ya Akili jana Dar es Salaam, Ummy pia alitaka huduma za afya ya akili na wataalamu zipatikane kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali ya taifa na kuwe na vituo vya huduma hizo.

“Ni kwa nini bima ya afya zisikubali kugharamia afya ya akili? Kama tunaruhusu watu kwenda kwenye matibabu kwa nini huduma za kisaikolojia na huduma zingine za afya ya akili zisiwe kwenye huduma za bima ya afya?” Alihoji Waziri wa Afya.

Alisema magonjwa ya akili yameongezeka na takwimu za kidunia zinaonesha kati ya watu wanane mmoja ana tatizo la akili, na Tanzania inakadiriwa kuwa watu milioni saba wana tatizo hilo huku watu milioni 1.7 wakiwa na sonona.

Alisema magonjwa ya akili yaliyopo kwa kiasi kikubwa ni sonona, kihoro, sifenia, matumizi ya bangi na pombe.

Alisema watu milioni 1.5 wanaishi na sonona wengi wao wakiwa ni wanawake, huku kukiwa na vitendo vya kikatili ndani ya jamii na ongezeko la takwimu za ubakaji na ulawiti.

“Unajiuliza huyu mtu ana akili timamu, tumeona takwimu za watoto kujiua na tumeambiwa na WHO kifo kimoja kati ya vifo 100 hutokana na kujiua, kwa hiyo asilimia 50 ya kesi hizo zinatokea kabla umri wa miaka 50, matukio ya kujiua ni sababu ya nne ya vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 29,” alibainisha Ummy.

Alisema mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika kutengamaa katika kufikiri, hisia na anavyotambua mambo katika matendo yake ya kila siku na kushirikiana na jamii na mahali pa kazi.

“Kuna uhusiano kati ya afya ya akili na ukuaji wa uchumi wa katika ngazi ya mtu mmojammoja, familia, jamii na taifa kwa ujumla, lakini yapo magonjwa ya akili ambayo yanaathiri na kuleta mabadiliko katika kufikiri, kuhisi na kutenda na hivyo kuwa na mabadiliko ya kitabia na kushindwa kuendana na jamii husika,” alisema.

Aliongeza: “Bila afya ya akili hakuna afya, lakini tunaogopa tunajificha katika kivuli cha unyanyapaa. Tutasikiliza kutoka kwa wachokoza mada tutaangalia tatizo la afya katika jamii, shuleni, afya ya akili kwa watoto, binafsi kama waziri nimeona tuvunje ukimya.”

Ummy alisema tatizo la afya ya akili ni kubwa kwani sasa kuna wanawake wengi kwenye vipochi vyao wanatembea na maji ya baraka na mafuta ya upako.

“Lakini kushamiri kwa makanisa mengi ya ajabu ajabu ni changamoto ya afya ya akili,” alisema.

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Mwanaidi Ally alisema kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (Tamisemi), wamejenga uwezo kwa halmashauri 73 na kamati za ulinzi na usalama kwa mwanamke na mtoto katika kutoa huduma za kisaikolojia na huduma za afya ya akili.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma ya Maendeleo ya Jamii, Stanslaus Nyongo alisema kuna tatizo kubwa la afya ya akili katika jamii.

Habari Zifananazo

Back to top button