DAR ES SALAAM: WAZIRI wa Afya,Ummy Mwalimu ametoa tahadhari ya wananchi kuepuka kutiririsha maji taka kuelekea msimu wa mvua za masika na kuzitaka halmashauri kuweka sheria kali za faini ili kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu nchini.
Ummy amesema kasi ya ugonjwa wa kipindupindu imepungua nchini ambapo ni mikoa miwili pekee inapata kesi mpya ambapo awali mikoa 10 ilikubwa na ugonjwa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jiji Dar es Salaam Ummy alisema bado kunachangamoto ya mlipuko wa kipindipindu ambapo kesi mpya zinatoka katika mikoa ya Mwanza na Simiyu.
“Lakini habari njema ni kwamba takwimu zangu za leo mpaka saa sita usiku jana tumebakiwa na mikoa miwili tu kwa upande wa Mwanza tumebakiwa na manispaa ya Ilemela na Simiyu tuna bariadi Dc na Meatu tunashukuru kwasababu tulikuwa na mikoa 10 ambayo inaripoti wagonjwa wapya wa kipindupindu sasa imebaki hiyo.
Ummy ameeleza kuwa wanaendelea kuhimiza wananchi kuzingatia kanuni za usafi binafsi na usafi wa mazingira ambapo wiki ijayo watazindua kampeni itakayojikita kwenye masuala ya afya ,mazingira kwani wakiweka mazingira safi na salama wataweza kupambana na kipindupindu.
Aidha ametoa wito kwa majiji hususan Dar es Salaam na Mwanza kwa msimu wa mvua kudhibiti utiririshaji wa maji taka kwa kuweka sheria kali kwa wote watakaotiririsha maji taka barabarani na makazi ya watu.