Ummy: NHIF haitatetereka, wadanganyifu kikaangoni

SERIKALI imesema haitakubali Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) utetereke, na imetoa siku 14 kwa mfuko uwasilishe mpango wa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kudhibiti udanganyifu.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alitoa agizo hilo jana Dodoma, akisema serikali haitakubali NHIF itetereke na akaonya watoa huduma waache udanganyifu huo.

Ummy aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kuanzia sasa hawatamvumilia mtoa huduma mwenye vitendo vya udanganyifu kwa kuwa asilimia 70 ya mapato ya hospitali ni fedha kutoka mfuko huo wa serikali.

“Jamani msione hivi…kuna uhuni unafanyika na ndio maana tumesema hatutakubali mfuko huu utetereke, utasimama imara kwa kuchukua hatua,” alisema Ummy.

Aliongeza: “Nyingine ni wataalamu wetu sisi, leo unaenda kwenye kituo cha afya cha serikali yule mtaalamu anakuambia kesho njoo kwenye kituo changu, ndo maana tunaweka gavana.”

Aliagiza watoa huduma wazingatie mifumo ya serikali na tabia ya kuhamisha wagonjwa iachwe.

“Maana watu wanahamisha wagonjwa, hivi mtu umefika Ocean Road halafu kesho asubuhi unaenda kwenye ka- kliniki, ugonjwa huohuo, vipimo hivyo hivyo, mtaalamu huyo anaenda kukutumikia,” alieleza waziri.

Ummy pia alisema kumekuwa na udanganyifu kwa wanachama kuwatoa wategemezi wakiwamo watoto na kuwaingiza watu wengine ambao ni wagonjwa.

“Kuna mwingine anamtoa mtoto kisa haumwi halafu anamuingiza baba mkwe mgonjwa…maana ya bima ya afya wengi wanachangia kwa ajili ya wachache wanaoumwa,” alifafanua.

Aidha, alisema kumekuwa na changamoto ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama kisukari, presha, moyo, saratani na mengineyo.

“Mimi ni Waziri wa Afya sio waziri wa wagonjwa…jukumu la kwanza ni kuwakinga wananchi ili wasiumwe,” alisema Ummy na kubainisha kuwa ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza limesababisha NHIF kuelemewa na gharama za tiba.

Akitoa mfano, alisema gharama za wagonjwa wa saratani na riba ya mionzi kwa mwaka 2015/2016 ilikuwa ni Sh bilioni tisa na mwaka 2021/2022 imefikia Sh bilioni 22.5.

Pia gharama za matibabu ya figo mwaka 2015/2016, mfuko ulilipa Sh bilioni 9.5, mwaka 2021/2022 umelipa Sh bilioni 35.4 na kwa wagonjwa wa moyo mwaka 2015/2016 mfuko umelipa Sh milioni 500 na mwaka 2021/2022 ulilipa Sh bilioni 4.38.

“Lazima tuongeze jitihada kwenye huduma za kinga badala ya tiba kwa kufanya mazoezi, kuangalia vyakula tunavyokula, kupunguza matumizi ya chumvi kupita kiasi, sukari, mafuta, kujiepusha na matumizi ya pombe kupita kiasi na kuzingatia lishe bora,” alisema Ummy.

Alisema wakati NHIF inaanzishwa ilikuwa kwa ajili ya watumishi wa umma pekee, lakini baadaye kukawa na mfumo wa kuingiza wanachama kujiunga kwa hiari.

“Asilimia 99 wanaojiunga na NHIF kwa hiari ni wagonjwa, anajiunga baada ya mwezi mmoja anaanza kupata matibabu,” alieleza.

Alisema kwenye Toto Afya kuna wanachama takribani 180,000 ikiwa ni idadi ndogo kwani sasa watoto wako milioni 20.

“Wakijiunga watoto hata milioni tano watasaidia wengine sasa watoto wengi wanazaliwa wakiwa na magonjwa mbalimbali…mtoto anajiunga kwa bima ya shilingi 50,400 lakini operesheni anayofanyiwa ni shilingi milioni 1.2, lazima tuhamasishe wengi zaidi wajiunge ili kuweza kuimarisha mfuko,” alieleza Ummy.

Alisema kwa sasa NHIF ina wanachama milioni 4.8 hivyo ni muhimu wananchi wengi wajiunge ili fedha za kutosha zipatikane kwa ajili ya kuuendesha mfuko.

Habari Zifananazo

Back to top button