Ummy: Tunajikita katika huduma bora kwa watoto wachanga
TANGA: TAASISI ya Doris Mollel Foundation kwa kushirikiana na Msanii maarifu Barnaba imetoa Vifaa Tiba kwa ajili ya kuanzisha Wodi ya Watoto Wachanga Mahututi (Neonatal Intensive Care Unit) ikiwemo watoto njiti katika Hospitali ya Masiwani, Halmashauri ya jiji la Tanga.
Akipokea vifaa hivyo, Mbunge wa Tanga Mjini na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kuwa, mwelekeo wa serikali ya awamu ya sita kwa upande wa afya ya uzazi, Mama na Mtoto ni kujikita katika utoaji wa huduma bora kwa watoto wachanga hususani watoto wanaozaliwa kabla ya wakati (njiti) ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Ummy ameipongeza na kuishukuru Taasisi ya Doris Mollel Foundation kwa kuwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dk Samia Suluhu za kuhakikisha Tanzania inafikia Malengo Endelevu ya Milenia ya kupunguza vifo vya watoto wachanga hadi kufikia vifo 12 kwa kila vizazi hai 1,000 ifikapo mwaka 2030 kutoka vifo 24 kwa kila vizazi hai 1,000 kwa sasa.
Vifaa tiba hivyo vimetolewa kwa lengo la kupunguza rufaa na kuwasaidia watoto hao kupata huduma bora karibu na jamii alipozaliwa kama alivyoeleza Mkurugenzi wa Taasisi ya Doris Foundation Doris Mollel.
Kulingana na tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa watoto wachanga karibu asilimia 50 hupoteza maisha wanaposafirishwa umbali mrefu kwa sababu ya kupoteza joto la mwili.
Vifaa vilivyotolewa na Doris Mollel Foundation ni pamoja na vitanda vya hospitali viwili, mashine ya mwanga ya kutibu manjano moja, mashine ya kusaidia mtoto mchanga kupumua moja, puto la kumsaidia mtoto kupumua moja,
Mashine ya joto, magodoro ya kuongeza joto la mtoto, mashine za kutolea dawa kusaidia kupumua, mashine ya kupima kiwango cha oxygen kwa mtoto . Pump za miguu, Pump zaa umeme,
Mashine za kutengeneza oxygen na mizani ya kupima uzito wa watoto, Vifaa hivyo vina thamani ya Sh milioni 35.
Akizungumzia baada ya kupokea vifaa hivyi, Ummy nae amemtaka Mkurugenzi wa Jiji la Tanga kuhakikisha Hospitali ya Jiji inaanzisha haraka Wodi ya Watoto Mahututi katika Hospitali hiyo.
Wakati huo huo, Taaasisi ya Mollel imekabidhi zawadi ikiwemo mabeseni ya watoto,kwa wanawake 50 waliojifungua katika Hospitali ya Jiji Masiwani, Kituo cha Afya Makorora, Kituo cha Afya Ngamiani na Kituo cha Afya Mikanjuni.