KUTII sheria bila shuruti ni msemo uliozoeleka maeneo yote kutokana na kampeni iliyokuwa ikifanyika ya kuzuia uhalifu na kuwataka wale wenye vitendo viovu wajisalimishe.
Hivyo baadhi ya madereva ambao wamekuwa wakibeba mizigo iliyopitiliza uzito wanatakiwa watii sheria bila shuruti ili kuepuka uharibifu wa miundombinu ya barabara.
Imebainika magari yanayobeba mchanga, kokoto na mawe hayapiti kwenye mizani wakati yamezidisha uzito na kuchangia uharibifu wa barabara.
Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, Samweli Anthony na Jumanne Ally, kwa nyakati tofauti wanasema kuwa madereva wamekuwa wakikwepa kupita kwenye mizani na kutumia njia za panya kufikisha mizigo waliyobeba.
Anthony anasema wamekuwa wakiharibu barabara za mitaani kwa kukwepa kwao mizani na kuzifanya ziwe na mashimo na uharibifu huo hata kwenye barabara zinazomilikiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS).
Salum Iddi, ambaye kitaaluma ni dereva, anasema hakua anajua kama akibeba kokoto, mawe na mchanga atahitajika kupima kwenye mizani kama magari mengine ya kubeba mzigo kwani hutoa mchanga mtoni moja kwa moja na kupeleka eneo la ujenzi.
Mwenyekiti wa madereva wa malori ya kubeba mchanga, kokoto na mawe Manispaa ya Shinyanga, Samweli James, anasema maeneo mengi wanakotoa mchanga na wanakopeleka hayana mizani ya kupima.
“Tunafahamu sheria ya kupita gari kwenye mizani kama kuna madereva hawafahamu ni wachache, ila tuko tayari mkituwekea mizani maeneo ambayo hayana, tutapima,” anasema James.
Anasema kuwa kuna madereva wa malori ya kubeba mchanga, kokoto na mawe takribani 35 hivyo wataelimishana na kutii sheria iliyopo.
Ofisa uelimishaji kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Heiga Mfuruki, anasema kutotii sheria kwa kubeba uzito uliopitiliza ndiyo mwanya wa rushwa na kuiletea hasara serikali.
“Hivi ukibeba mzigo wako eneo lolote na kupita mizani kama sheria inavyotaka hakuna mtu atakayekusumbua, wewe dereva utakuwa umetekeleza sheria na kuiacha barabara ikiwa salama,” anasema Mfuruki.
Mwakilishi wa Jeshi la Polisi kutoka Kitengo cha Usalama Barabarani, Analyse Kaika anasema kuwa baadhi ya ajali zinatokea kwa kuzidisha mizigo na unachangia uharibifu wa barabara sababu lami itachubuka pia pale mafuta ya gari yanapomwagika.
Rebecca Marando, mhandisi kutoka Tanroads mkoani Shinyanga aliyetoa elimu kwa madereva anasema mkoa una vituo viwili vya mizani, eneo la Mwendakulima upande wa Kahama na Tinde mkoani Shinyanga.
“Ipo mizani ya kupima uzito wa magari na kuna za aina mbili ambapo ya kuhamishika na isiyohamishika na mfumo wa kupima gari likiwa kwenye mwendo na faini hutozwa kulingana na makosa yalivyo,” anasema Marando.
Meneja wa Tanroads mkoani Shinyanga, Mibara Ndirimbi anasema kuwa katika utunzaji wa barabara wamekuwa wakifanya kazi ya matengenezo ya barabara mara kwa mara.
Ndirimbi anasema kuwa katika bajeti ya mwaka 2022/2023, wametenga Sh bilioni 12.6 kwa ajili ya matengenezo ya barabara na kwa mwezi takribani magari 70 yamekuwa yakikamatwa kwa kuzidisha uzito.
“Yapo magari yanayobeba kwa kuzidisha uzito na bila kupita mizani, ninachowaomba madereva wa magari hayo mpite mizani kwa mujibu wa sheria iliyopo siku zoezi litakapofanyika la kupima uzito na ukibainika hatua kali zitachukuliwa,” anasema Ndirimbi.
Ndirimbi anasema shughuli za udhibiti uzito wa magari zinaendeshwa kwa mujibu wa sheria na kanuni hivyo kama kuna changamoto hiyo kwa madereva wa malori ya mchanga mizani zipo zinazohamishika, watafanya kazi hiyo.
“Tanzania ikiwa ni nchi mojawapo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki imeridhia Sheria ya Udhibiti Uzito wa Magari ya Jumuiya hiyo iliyopitishwa mwaka 2016 na kanuni zake za mwaka 2018,” anasema Ndirimbi.
Ndirimbi anasema kupitia sheria hiyo na kanuni zake magari yanapaswa kupimwa uzito kwa mujibu wa sheria ya udhibiti uzito wa mizigo kwenye magari.
Anasema sheria hiyo inamtaka msafirishaji kuhakikisha gari lake linapokuwa kwenye shughuli za usafirishaji linapimwa uzito katika mizani.
“Ujenzi wa miundombinu ya barabara na matengenezo unagharimu fedha nyingi takribani zaidi ya shilingi bilioni moja kutengeneza daraja pekee,” anasema Ndirimbi.
Anasema shughuli za udhibiti uzito wa magari hufanyika ili kuhakiki magari yanayoanzia tani 3.5 yanakuwa na uzito unaokubalika kisheria na uzito unazuiliwa sababu unafanya uharibifu wa barabara na madaraja.
Ndirimbi anasema uzito wa mzigo kwenye magari uliozidi huchangia barabara kuchoka na kuharibika kabla ya muda uliopangwa kiusanifu.
“Utozaji wa tozo za kuzidisha uzito hufanyika kwa magari yote yanayobainika kuzidi uzito na msafirishaji hutakiwa kutimiza masharti kwa mujibu wa sheria na kanuni husika,” anasema Ndirimbi.
Anasema kwa magari ambayo yanalazimika kubeba mizigo ambayo imezidi uzito unaokubalika kisheria na haiwezi kupunguzika ni ile mizigo iliyokidhi vigezo na kubebwa kwa kulipiwa tozo ya kuzidisha uzito.
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amewataka wasimamizi wa mizani inayosimamiwa na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), kutenda haki kwa wasafirishaji hasa wanapokutwa na makosa ya kuzidisha uzito.
“Sheria inayosimamia mizani ya Afrika Mashariki ni kali na ina tozo kubwa, hivyo hakikisheni mizani zinakuwa katika vipimo sahihi ili kuondoa mkanganyiko wa uwiano wa mizani unaojitokeza mara kwa mara,” anasema Profesa Mbarawa.
Mbarawa ametoa agizo mapema mwaka huu kwa ofisi zote za Tanroads nchini kuhakikisha wanaendelea kutoa elimu za mara kwa mara kwa watumishi wa mizani, wasafirishaji na madereva kuhusu sheria ya mizani.
Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania ambaye ni mwandishi wa habari mwandamizi, Marry Mwita anasema kuwa zipo sheria nzuri ambazo wananchi wanapaswa kuzifuata ili kuondoa changamoto kuendelea kulipatia taifa hasara.
“Sheria zote lazima zipitie bungeni na kama kuna sheria mbovu ambazo zimepitishwa na Bunge na zinawakandamiza wananchi lazima Bunge tena likae na kuzipitia upya sheria hizo na kanuni zake,” anasema Mwita.