Umuhimu soko la kaboni kukabili mabadiliko tabianchi

KWA sasa dunia inakabiliwa na ongezeko joto la wastani ambapo katika mwaka wa 2019 lilikuwa nyuzijoto 1.1. Kwa mujibu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), hii ni ya juu kuliko kipindi cha kabla ya viwanda.

Ili kudhibiti ongezeko la joto lisizidi nyuzijoto 1.5, inahitajika kupunguza uzalishaji wa gesi chafu kwa asilimia 7.6 kila mwaka kuanzia mwaka huu hadi 2030.

Kumekuwa na upungufu wa barafu, ukame, mafuriko na mabadiliko mengine kutokana na gesi za ukaa zinazozalishwa kwa shughuli za binadamu ambapo asilimia 30 ya idadi ya watu ulimwenguni wanakabiliwa na joto.

Upandaji miti unasaidia kupunguza hewa ukaa

Kwa mujibu wa WMO, wastani wa joto kwa kipindi cha miaka mitano (2015-2019) na kipindi cha miaka 10 (2010-2019) ndio ya juu zaidi kuwahi kurekodiwa.

Asilimia 70 ya nishati inayozalishwa duniani ni nishati chafu ambapo Afrika inakabiliwa na mabadiliko ya haraka ya madhara kutokana na kuwa karibu na mstari wa Ikweta uliopo karibu na jua.

Hata hivyo, Afrika inazalisha hewa ukaa kwa asilimia nne tu huku mabara mengine yakizalisha asilimia 96 ya hewa hiyo inayochochea mabadiliko ya tabianchi yanayoleta madhara kwa binadamu, mimea, wanyama, mazalia ya uoto na viumbe.

Kwa kuzingatia hili mataifa yaliahidi kupunguza uzalishaji wa gesi zinazochafua mazingira na kutumia nishati ambazo ni salama kwa tabaka la ozone.

Zaidi ya nusu ya Pato la Taifa (GDP) duniani hutegemea mazingira kwa kiwango cha juu hivyo kuwekeza kwenye suluhisho ya mazingira hakutapunguza tu ongezeko la joto ulimwenguni lakini pia kutasababisha mapato takribani ya Dola za Marekani bilioni nne kwa wafanyabiashara kubuni vitu vipya na ajira zaidi ya milioni 100 kila mwaka kufikia 2030.

Hewa ukaa inayotoka viwandani

Mataifa yalikubaliana kujitolea kisheria mjini Paris (Mkataba wa Paris) ambapo kupitia mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi ujulikanao kama COP kupunguza kiwango cha joto ulimwenguni kisizidi nyuzijoto mbili zaidi ya viwango vya kabla ya viwanda lakini pia yalitoa ahadi za kupunguza au kuzuia uzalishaji wa gesi ya ukaa kufikia mwaka wa 2030.

Kanuni za kupunguza kaboni

Matumizi ya nishati chafu yana nafasi kubwa kuzalisha hewa ukaa ambayo inaleta uharibifu wa tabaka la ozoni huku biashara ya kaboni ikitajwa kudhibiti mabadiliko.

Tanzania imeandaa kanuni ya udhibiti na usimamizi wa biashara ya kaboni ya mwaka 2022 kuweka mazingira ya haraka kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Biashara ya kaboni maana yake ni kuuza na kununua viwango vya kaboni vilivyoidhinishwa au kuthibitishwa katika utoaji, upunguzaji na uondoaji wa kaboni kwa mujibu wa viwango vya kaboni vya kimataifa.

Upandaji miti unatumika kama kigezo kikubwa kwani inafyonza hewa ya kabondioksaidi iliyopo katika tabaka la ozone na mhusika wa mradi baada ya vipimo atalipwa kutokana na ufyonzwaji wa hewa hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo anasema serikali inatarajia kunufaika na takribani Sh trilioni 2.44 kwa mwaka kutokana na biashara ya kaboni.

Dk Jafo anasema pamoja na kukuza uchumi wa nchi pia mapato hayo yatasaidia kupambana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi nchini.

Anasema kutokana na umuhimu huo, serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa biashara ya kaboni na tayari eneo la ekari milioni 48.1 limeshatengwa kwa ajili ya biashara hiyo.

Dk Jafo anafafanua tangu ofisi hiyo iandae kanuni na mwongozo huo idadi kubwa ya wawekezaji wa biashara ya kaboni wamejitokeza ambapo Kituo cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) kilichopo mjini Morogoro kimesajili kampuni 21 zinazojihusisha na biashara ya kaboni.

“Ni matarajio yetu biashara ya kaboni itasaidia kupunguza kiwango cha gesijoto kwa asilimia 30 hadi 35 hivyo tutaendelea kuongeza nguvu katika kushirikiana na wadau kufanikisha hatua hii,” anaeleza.

Kwanini soko la kaboni ni muhimu

Biashara ya kaboni ni soko la hiari lililozinduliwa wakati wa COP27 nchini Misri ambapo inalenga kuharakisha maendeleo ya kiuchumi huku ikipunguza hewa chafu kwani inalenga kuvutia Dola za Marekani bilioni sita kwa2030.

Biashara hiyo imewasilishwa kama fursa kuu ya ufadhili wa hali ya hewa kwa nchi nyingi za Afrika ikilenga kilimo, nishati na mifumo ikolojia ambapo hadi sasa kuna nchi saba za Afrika ambazo zimeunga mkono mpango huo.

Akizungumza na HabariLEO, Mkuu wa masuala ya Mpito ya Nishati ya Utafiti  kutoka Taasisi isiyo ya serikali ya Power Shift Africa, Amos Wemanya anasema mpango huo wa biashara ya kaboni bado ni mgeni Afrika.

Anasema mpango mwingine wa kukabiliana na hewa ukaa ni kukuza matumizi ya vyanzo vya nishati safi ikiwemo uzalishaji wa umeme unatokana na jua, upepo, umeme wa maji, jotoardhi au majani.

Mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri mazingira

“Kwa suluhu ya asili miradi inazingatia mbinu za mfumo wa ikolojia kama vile kilimo, misitu na urejeshaji wa ardhioevu na miradi safi ya jiko inapatikana.

” Changamoto soko la kaboni Wemanya anasema maendeleo ya masoko ya kaboni Afrika yanahatarisha matumizi ya ardhi na rasilimali zingine  barani humo ili kuwezesha nchi tajiri na mashirika yanayochafua mazingira kuendeleza viwango vya juu vya uchafuzi wa hali ya hewa ambao unaharibu Afrika.

“Kupanda misitu mipya kunahitaji ardhi na wale ambao tayari wanaishi na kutumia ardhi hiyo wanahofia ardhi yao inaweza kuchukuliwa na wasiwasi huo unaathiri haki za binadamu umekumba masoko ya kaboni,” anafafanua.

Afrika inahitaji hili  Wemanya anaeleza Afrika ina mahitaji ya haraka ya ruzuku na ufadhili wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi  kutoka vyanzo mbalimbali.

Mkuu wa masuala ya Mpito ya Nishati ya utafiti kutoka Taaisisi isiyo ya serikali ya Power Shift Africa, Amos Wemanya.

“Ilikadiria kwa Afrika pekee, gharama za kukabiliana na hali hiyo zinaweza kufikia Dola za Marekani bilioni 50 kwa mwaka ifikapo 2050 na gharama za kukabiliana na mabadiliko ya kuingia kwenye nishati safi zimekadiriwa karibu dola bilioni 125 kwa mwaka kati ya 2026-2030.”

COP27 haijafikia matarajio Afrika  Mwenyekiti wa Kundi la Afrika la Wazungumzaji wa Mabadiliko ya Tabianchi (AGN), Ephraim Shitima anasema kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi siku zote imekuwa kipaumbele cha kwanza kwa Afrika kwa sababu ya madhara makubwa na hatari kwa bara hilo.

Shitima anasema katika mkutano wa COP27 nchi nyingi zikiwemo Afrika ziliangazia hitaji la dharura kwa mabadiliko hayo kwa jamii na sekta zilizo katika mazingira magumu.

“Hata hivyo, matokeo ya kukabiliana na hali ya mabadiliko kupitia COP27 hayajafanikiwa kama ilivyokusudiwa na kutokuwa na matarajio ya kutosha kulingana na mahitaji ya nchi za Afrika,” anasema Shitima.

*Makala haya imewezeshwa na MESHA na Ofisi ya Afrika ya IDRC Mashariki na Kusini.

 

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button