UN yataka migogoro imalizwe

UMOJA wa Mataifa (UN) umeitaka Serikali ya Sudan Kusini na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua mapema kukomesha kusambaa kwa chuki na migogoro nchini na kunakoleta athari kubwa kwa wananchi.
Mtaalamu wa masuala ya haki za binadamu aliyeteuliwa na Umoja wa Mataifa nchini, Yasmin Sooka ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Sudan Kusini, alisema kama hatua za haraka hazitachukuliwa, hali itakuwa mbaya katika siku za usoni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Haki za Binadamu iliyopo mjini Juba, Sooka akishirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa, ataendelea kutoa ujumbe kwa nchi na jumuiya ya kimataifa pamoja na serikalini ili kupambana na viashiria vya kueneza mgogoro.
“Bila kuchukuliwa kwa hatua hizo, kuna hatari ya kushuhudia mamilioni mengine ya wananchi wa Sudan Kusini wakiyakimbia makazi yao au kuvuka mipaka ya nchi kwenda nchi jirani kutafuta makazi,” alisema Sooka.