DSM: Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Mloganzila, Oktoba 27, 2023 itaendesha upasuaji wa kutengeneza shepu ‘cosmetics surgery’ kwa watu wenye uhitaji wa kupunguza tumbo na kuchonga kiuno, wenye kutaka kuongeza matiti, kupunguza matiti, ,kupunguza mikono, kuongeza makalio na kadhalika.
Akizungumza na HabariLEO, daktari bingwa wa upasuaji Erick Muhumba amesema upasuaji huo utafanyika kwa siku moja kwa kushirikiana na madaktari wabobezi kutoka India.
“Ni mara ya kwanza kwa Tanzania kufanya upasua rekebishi ambao lengo ni kupunguza uzito, tunamanisha upasuaji wa tumbo ambao tunapunguza nafasi ya kuhifadhi chakula,” amesema.
Amesema, kuna aina tatu ya upasuaji ambao ni kukata sehemu ya tumbo na kuliondoa, upasuaji mwingine ni ‘Bypass’ ambao unavuka sehemu ya kuhifadhi chakula na chakula kinapita kwenye koo na kwenda kwenye utumbo mdogo.
“Njia ya tatu hii ndio ya kisasa zaidi ambayo tunaingiza kifaa mdomoni na kukishusha ndani ya tumbo na kushona,” amesema.
Dk Erick amesema kwa kuanza watafanyia upasuaji rekebishi watu watano na kwamba mpaka sasa wawili wameshalipia na wanasubiri huduma.
“Bado watatu, ila kama muitikio utakuwa mkubwa zaidi basi tutaongea na wenzetu wabobezi waongeze siku, ili kukidhi mahitaji ya wateja wetu,” amesema.
Amesema gharama za kufanya upasuaji wa tumbo ni dola za Marekani 8,000 ambazo ni sawa na Sh milioni 20, kupunguza mikono, maziwa, matiti na upasuaji mwingine wowote wa kurekebisha shepu ni dola 7,000 sawa na Sh milioni 17,500,000
“Gharama hizi ni nafuu zaidi kuliko gharama ambazo mtu anazitumia kwenda nje ya nchi, hata hivyo kuna nafasi ya mazungumzo, ili kupunguza kiasi kidogo cha gharama,” amesema Dk Erick.
Comments are closed.