Klabu ya Yanga imefikia tamati leo ya kucheza michezo 49 bila kufungwa baada ya kupokea kipigo cha kwanza cha mabao 2-1 kutoka kwa Ihefu FC na kushindwa kufika michezo 50. Mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Highland Estate Mbeya.
Mara ya mwisho timu hiyo kufungwa ilikuwa mwaka 2021 dhidi ya Azam FC, bao la Prince Dube. Licha ya kufungwa bado Yanga inaendelea kuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 32 sawa na Azam FC yenye mchezo mmoja mbele.
Mabao ya Ihefu yalifungwa na Never Tigere dakika ya 39,kwa mkwaju wa Faulo na Kenny Kissu kwa mpira wa kona dakika ya 62. Bao la Yanga limefungwa na Yannick Bangala dakika ya tisa ya kipindi cha kwanza.
Yanga sasa imebakiwa na mchezo mmoja mkononi, ambapo mpaka sasa amecheza michezo 13, Azam na Simba wakiwa na 14. Baada ya mchezo huo kuchezwa timu zote zitakuwa sawa.