Ulezi, mtama ni tiba uzito mkubwa

TATIZO la uzito uliopitiliza linaweza kupata ufumbuzi kwa kutumia unga wa mtama kwa kuchanganya na ulezi katika vyakula mfano ugali au uji kutokana na kuwa na kiwango kidogo cha sukari pamoja na wanga.

Mtafiti Mwandamizi Usindikaji na Uongezaji Thamani kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI) , Kituo cha Ukiriguru Mwanza, Dk Caresma Chuwa,amesema hayo alipozungumzia faida ya zao la mtama kwenye maonesho ya Nanenane yanayoendelea viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya.

“ Kwa wagonjwa wa sukari unapokula mtama kuna kemikali inayoitwa ‘tanning’ ambayo inazuia umeng’enywaji wa virutubishi vingine na kusababisha ule ugali wa mtama uweze kukaa kwa muda mrefu tumboni na husikii njaa, kwa kuwa umeng’enywaji wake unachukuwa muda mrefu na utaacha kula vyakula vingine ikasababisha ukaongezeka uzito,” amesema.

Advertisement

Amesema mtama ndio zao ambalo lina kiwango kidogo cha sukari ukilinganisha na mchele na ngano, hivyo ili kupunguza uzito mtu anatakiwa kula sukari isiyozidi gramu 250 kwa siku kuanzia mlo wa asubuhi mpaka jioni, hivyo ukitumia vyakula unga wa mtama au ulezi kupikia ugali au uji kwa siku utaepuka kuongeza kiwango cha kuwa na uzito uliopitiliza.

“Ili kuweza kupunguza uzito inatakiwa mtu ale sukari isiyozidi gramu 250 kwa siku yaani ina maana kuanzia chakula cha asubuhi ukila mkate vipande vitatu ni sawa na gramu hizo 250 inatosha, lakini ukila chapati tatu asubuhi,mchana ukila ugali wa sembe na jioni wali hivyo kiwango cha sukari kitakuwa kimezidi kwa siku na kukaribisha ugonjwa wa sukari na uzito uliopitiliza,’ amesema.

Amesema endapo mtu ataendekeza utaratibu wa kula hivyo atakuwa anaongeza kiwango cha sukari na kufikia gramu 800 mpaka 1000 kwa siku,

Hivyo jinsi mtu anavyoendelea kula sukari na anavyokuwa ndio anakaribisha tatizo la uzito na ugonjwa wa sukari kutokana na kuzidi katika damu na kongosho linashindwa kuondoa sukari ya ziada.

“ Sasa jambo hilo la uzito uliopitiliza lisiweze kutokea tunatakiwa sasa kurudi kwenye vyakula vya mazao ya nafaka ambayo mtama na ulezi yanasaidia kuepuka tatizo hilo,” amesema.

Alisema kwa upande wa mazao ya mizizi wanahamasisha watu wale viazi mviringo na ndizi hasa wakati wa jioni kwa kuwa vyakula hivyo vina kiwango kidogo cha wanga na endapo atakula vyakula vyenye wanga mwingi na kulala ule umeng’enyaji wa sukari unaingia kwa kiwango kingi kwenye damu na hivyo kupata matatizo hayo.

Alivitaja vyakula vinavyoweza kutengenezwa kwa kutumia mtama ili kuepuka uzito kwa kuchanganya mahindi na ngano, jamii ya mikunde yenye protini nyingi ili kuongezea virutubishi, ili kupata afya bora kwa kutengeneza vyakula kama togwa, mbege, uji ,biskuti, maandazi na mikate.

mwisho

2 comments

Comments are closed.