Unicef yaeleza hatari kwa watoto kuzaliwa njiti

MTOTO mmoja kati ya kila watoto 10 huzaliwa njiti na kila baada ya sekunde 40, mtoto mmoja kati ya hao hufariki dunia.
Hayo yamebainishwa katika ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) ya Mei 10 mwaka huu inayoeleza kuwa watoto milioni 150 walizaliwa njiti katika muongo uliopita.
Unicef inasema kuwa takribani watoto milioni 13.4 walizaliwa njiti mwaka 2020, huku milioni moja kati yao, walifariki dunia kutokana na matatizo ya kuzaliwa kabla ya wakati.
“Athari za migogoro, mabadiliko ya tabianchi, Covid-19 zinaongezeka hatari kwa wanawake na watoto kila mahali, hatua za haraka zinahitajika ili kuzuia watoto kuzaliwa kabla ya wakati, pamoja na kuimarisha huduma boara kwa watoto na familia zao,” inasema Unicef.
Kwa mujibu wa Unicef, tatizo la watoto kuzaliwa kabla ya wakati linaongoza kwa kusababisha vifo vya watoto kwa kuwa kifo kimoja kati ya kila vifo vitano vya watoto, hutokea siku tano kabla ya kuzaliwa kwao.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kusini mwa Asia ndiko kunaongoza kuwa na kiwango cha juu watoto kuzaliwa kabla ya wakati na hukabiliwa na hatari kubwa ya kifo.
Ripoti hiyo inaonesha kuwa athari za migogoro, mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa mazingira, Covid-19 na kupanda kwa gharama za maisha kunaongeza hatari kwa wanawake na watoto.
“Kwa mfano, uchafuzi wa hewa unakadiriwa kuchangia watoto milioni sita kuzaliwa njiti kila mwaka. Takribani mtoto 1 kati ya 10 anayezaliwa kabla ya wakati anazaliwa katika nchi 10 zilizoathiriwa zaidi na majanga ya kibinadamu,” inasema Unicef.
Dk Nahya Salim kutoka Tanzania amenukuliwa kwenye ripoti hiyo akisema:” Sasa hakuna kisingizio cha kunyamaza. Mikononi tuna nyenzo na maarifa ya kubadilisha matokeo kwa watoto wetu wachanga walio katika mazingira magumu zaidi.
“Najivunia kuona serikali yangu inawekeza hata maeneo ya vijijini. Muongo ujao unaweza na lazima uwe wa tofauti kwa wale wanaokabiliwa na tatizo la kuzaliwa kabla ya wakati hapa nchini na kila mahali.”