Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF, limelaani shambulio lililofanyika katika Shule ya Sekondari Lhubiriha, iliyopo Mpondwe, wilaya ya Kasese, Uganda ambako wanafunzi 40 wameuawa huku wengine wakitekwa.
Mwakilishi Mkazi wa UNICEF nchini humo Dk Mohammed Munir Safieldin, amelaani mauaji hayo yaliyofanyika usiku wa kuamkia jana na kutaka kuachiliwa haraka wanafunzi waliotekwa, ambapo waasi wa kundi la ADF wanahusishwa na tukio hilo.
Dk Nadir amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha shule kwa wakati wote zinakuwa katika mazingira salama kwa walimu, wanafunzi na wote wanaohusika kutoa huduma mbalimbali.
“Ni lazima tufanye kazi pamoja bila kuchoka, ila kuhakikisha vitendo hivi vya ukatili haviharibu usalama wa taasisi zetu za elimu,” alisema Dk Nadir.
“Natoa pole kwa wafiwa wote ambao kwa sasa wanapitia machungu yasiyovumilika kutokana na kitendo hiko cha kikatili, naungana na watu wote wa Uganda kama ishara ya mshikamano katika wakati huu wa majonzi, “ aliongeza Dk Nadir.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, mlinzi wa shule hiyo aliuawa pamoja na wakazi wengine watatu wa eneo hilo, kabla ya bweni lenye wanafunzi katika shule hiyo kuchomwa moto, ambapo miili ya majeruhi pamoja na waliopoteza maisha imepelekwa katika hospitali ya Bwera wilayani humo.