UNICEF yatoa tamko mlipuko wa kipindupindu
SHIRIKA la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limetangaza hali ya dharura kwa watoto kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu mashariki na kusini mwa Afrika.
Katika taarifa yao, UNICEF imetoa wito wa ufadhili zaidi kusaidia sio tu kulinda watoto zaidi na jamii zinazohitaji lakini kubuni mifumo thabiti ya kulinda watoto katika siku zijazo.
Shirika hilo limeomba msaada wa dharura wa Dola milioni 171 kujibu mahitaji yanayoongezeka ya watu milioni 28, wakiwemo watoto na familia zao katika eneo lililoathiriwa na kipindupindu.
Fedha hizo zitatengwa kwa ajili ya utoaji wa huduma za maji ya kuokoa maisha, usafi wa mazingira na usafi, afya, lishe, ulinzi wa mtoto na huduma za elimu kwa wanawake na watoto walioathirika na mlipuko huo.
Shirika hilo limesema wakati wafadhili tayari wamechangia dola milioni 18.3 kusaidia kukabiliana na kipindupindu, pengo la ufadhili wa kikanda linahitaji kuzibwa haraka ili kukabiliana na hali iliyoibuka.