Unyanyasaji kijinsia waongeza wagonjwa wa akili

IMANI potofu pamoja na vitendo vya  unyanyasaji wa kijinsia katika maisha ya binadamu vimetajwa kuwa miongoni mwa mambo yanayochangia ongezeko la idadi kubwa ya wagonjwa wa akili katika jamii.

Hayo yamebainishwa wakati wa ufungaji wa kambi ya siku tatu ya kupima afya na maradhi yasiyoambukiza inayofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam chini ya Jumuiya ya Khoja Shia Ithnasheri.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo Tanzania, Mohamedraza Dewji alisema mbali na hilo pia msongo wa mawazo na mkwamo katika mahusiano, uchumi pia ni sababu nyingine inayosababisha hali hiyo.

Alibainisha kuwa mtu mmoja kati ya wanne hukumbwa na tatizo hilo kwa nyakati tofauti.

Aidha, alisema kuwa ugonjwa wa msongo wa mawazo ni chanzo namba mbili kwa vifo kwa vijana wenye umri kati ya miaka 19 hadi 29 na kuelezea kuwa asilimia 75 ya watu wanaokabiliwa na ugonjwa huo katika nchi zinazoendelea hawapati matibabu ya uhakika.

“Kwa kweli hali ya maradhi ya akili yanazidi kuwaathiri watu wengi na inadaiwa kuwa watu milioni 350 duniani wameathirika na msongo wa mawazo na kwa waathirika wengi hunyanyapaliwa kwa sababu ya kuwa na ugonjwa huo na hali hiyo huzuia watu wengi wenye maradhi hayo kukosa msaada,” alisema Mohamedraza.

Alisisitiza kupumzika na kuburudisha mwili kwa namna tofauti ikiwemo kufanya mazoezi na kula chakula kizuri ili kuepuka maradhi hayo.

Katika kuhitimisha kambi hiyo, jumuiya kwa kushirikiana na Taasisi za Fikra Afya Pamoja na The Awaited Rehab ya Kigamboni, wametoa mafunzo ya kukabiliana na msongo wa mawazo kwa washiriki zaidi ya 4,000 waliotembelea kambi hiyo na kuwataka kuipeleka elimu hiyo katika jamii.

Kila Oktoba 7, Tanzania huungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku ya kimataifa ya afya ya akili. Wadau wa afya hukaribishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kutoa elimu na kuhamasisha kuhusu ufahamu wa magonjwa hayo, tiba na hata kinga.

 

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x