Uongozi wa mabasi ya New Force watii amri

UONGOZI unaosimamia mabasi ya New Force umetii amri ya Mamlaka ya Udhibiti Usafi ri Ardhini (Latra) kuyazuia kuanza safari saa tisa usiku. Taarifa ya Kampuni ya New Force Enterprises Limited imeeleza kuwa kuanzia leo safari zote za mabasi hayo zitaanza saa 12 asubuhi.

Katika taarifa hiyo kupitia ukurasa wake wa twitter, kampuni hiyo ilitaja safari hizo ni za kutoka Dar es Salaam, Mbeya, Kyela, Songea, Tunduma na Sumbawanga.

“Na kwa Shekilango gari zitaondoka saa 11:00 kuelekea stendi ya Magufuli Mbezi,” ilieleza taarifa hiyo.

Juzi Latra ilitangaza kufuta ratiba za alfajiri kwa mabasi 38 ya kampuni ya New Force na kuagiza yaanze safari saa 12 asubuhi.

Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo alitangaza uamuzi huo baada ya kuzungumza na uongozi wa kampuni hiyo kutokana na kukithiri kwa ajali zinazodaiwa kusababishwa na uzembe wa madereva wa mabasi hayo.

“Hivyo kuanzia Julai 5, mwaka huu, mabasi yote 38 ya kampuni ya New Force yataanza safari zake saa 12 asubuhi na si saa tisa alfajiri wala saa 11 alfajiri.

“Hii si adhabu, ni hatua za udhibiti tumechukua kuhakikisha usalama wa abiria, chombo cha usafiri na mali,” alisema Suluo.

Alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na Latra ulibaini kuwepo na uvunjaji wa makusudi wa kanuni za usafirishaji wa magari ya abiria hasa wanaotumia ratiba ya saa tisa na saa 11 alfajiri.

“Unakuta dereva amethibitishwa na Latra lakini hatumii mfumo wa utambuzi wa dereva anapoendesha basi au wengine wanachezea mfumo wa kufuatilia mwenendo wa mabasi (VTS) na kwenda mwendo kasi zaidi na baadhi ya magari yaliyopata ajali yakiwemo ya kampuni hii yalikiuka kanuni na utaratibu na ndio sababu tunachukua hatua kudhibiti,” alisema Suluo.

Alisema kati ya Juni 6 na Julai 2, mwaka huu, mabasi ya kampuni ya New Force yalihusika katika ajali tano za barabarani na tatu kati ya hizo zilitokana na uzembe wa madereva wa mabasi hayo.

Suluo alisema kumbukumbu zinaonesha walishawahi kusitisha leseni sita za mabasi ya kampuni hiyo kwa kuwa madereva wake walikithiri katika ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Latra imeiagiza kampuni hiyo iwasilishe orodha ya madereva wake na namba za leseni zao na mamlaka hiyo itaendelea kufanya uchunguzi kwenye menejimenti ya kampuni hiyo ili kufahamu utaratibu wa ajira za madereva na namna wanavyowasimamia.

Meneja wa mabasi hayo, Masumbuko Masuke alisema kuna changamoto kwa madereva wao na wamepanga kuwaita na kuwarudisha tena mafunzoni kuanzia Jumamosi wiki hii.

Habari Zifananazo

Back to top button