Upanuzi mkongo kukuza uchumi wilaya 23

KUKAMILIKA kwa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kutaisaidia utekelezaji wa Tanzania ya kidijiti na kufungua fursa za kiuchumi na mawasiliano ya uhakika kwa wananchi katika wilaya 23, imebainika.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema hayo jijini Dodoma jana wakati wa kusainiwa mkataba wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Mkataba huo ulisainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Peter Ulanga na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huawei International, Demon Zhang.

“Mkataba huo ni wa ujenzi wa kilometa 1,520 ambazo zitaunganishwa katika mkongo kwenda katika wilaya 23 na utagharimu shilingi bilioni 37.4 ambapo mkataba huu unatakiwa kukamilika ndani ya miezi sita,” alisema Nape.

Alisema mradi huo utasaidia kukuza matumizi ya tehama na kuongeza upatikanaji wa intaneti yenye kasi.

Alisema kukamilika kwa mradi huo kutaondoa changamoto za mawasiliano katika wilaya 23 ambazo zitaunganishwa kwenye mkongo huo.

Alizitaja wilaya hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Msalala na Mbogwe (Shinyanga), Pangani, Muheza, Kilindi, Mombo na Lushoto (Tanga), Halmashauri ya Wilaya ya Ngara (Kagera) na Mwanga na Hai (Kilimanjaro).

Nyingine ni Karatu, Longido na Mbulu (Arusha), Kibiti (Pwani), Halmashauri ya Mtama, Ruangwa na Nachingwea (Lindi), Newala (Mtwara), Ludewa (Njombe), Mbinga (Ruvuma) na Vwawa na Ileje (Songwe).

Nape alisema mawasiliano kupitia mkongo huo yatasaidia wilaya hizo kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato kwa kutumia mifumo ya kidijiti na taasisi za umma na binafsi zitakuwa na uwezo wa kufikisha huduma zao kwa wananchi kwa haraka na wakati.

Alisema mikoa yote imeunganishwa katika mkongo na umefika katika vituo vya mipakani vinavyopakana na nchi jirani, hivyo Tanzania imekuwa nchi muhimu katika ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Alisema serikali itawafikia wananchi kwa urahisi kupitia mkongo huo kwani uwekezaji huo ni faida kwa ukuaji uchumi.

Alitoa rai kwa TTCL kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa mujibu wa mkataba na wajipange ili wadau wajiunge kwenye mkongo kupeleka huduma kwa wananchi.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya TTCL, Zuhura Murro alisema utiaji saini huo ni muhimu kwa TTCL na taifa kwa ujumla kutokana na uwekezaji huo ambao unaenda kuimarisha sekta ya mawasiliano na kuchangia katika kukua kwa sekta nyingine za maendeleo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button