Upanuzi Uwanja Ndege Mpanda waanza

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Tanzania(TAA), imeanza uboreshaji na upanuzi wa jengo la abiria katika Uwanja wa Ndege Mpanda, uliopo mkoani Katavi, ambao awali kulikuwa na changamoto ya ufinyu wa jengo hilo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC),imetembelea uwanja huo ili kujionea utendaji wake na baada ya hapo Mwenyekiti wa Kamati hiyo Jerry Silaa, amemuagiza mkandarasi anaetekeleza mradi huo kuwa mzalendo kwa kukamilisha mradi huo kwa mujibu wa makubaliano.

Silaa ameitaka TAA kumsimamia vizuri mkandarasi anaetekeleza mradi huo, ili uweze kukamilika kwa wakati hatimaye kuhudumia wananchi.

Advertisement

Ameipongeza serikali kwa ujenzi wa uwanja huo, ambao ni lango la uchumi kwa ukanda wa Magharibi mwa Tanzania kwa kurahisisha safari za anga, ambapo Shirika la Ndege la (ATCL), ndilo linalofanya safari zake mkoani humo na imechangia kufungua fursa mbalimbali za kibiashara.

“Mkoa wa Katavi umepakana na nchi ya Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo), kwenye lango la kibiashara niseme tuu uwanja huu wamepata mradi wa ukarabati wa jengo la abiria, ambalo tayari mkandarasi ameshakabidhiwa saiti tangu Machi 10, 2023,  kwa hiyo jengo hili litaboreshwa, tukija baada ya miaka miwili baadaye jengo hili litakuwa la kisasa,” alisema.

Kwa upande wake Meneja wa Uwanja wa Ndege Mpanda, Jeff Shantiwa amesema jengo la abiria lililopo sasa lina uwezo wa kuchukua abiria 48, huku ndege inayokuja inachukua abiria zaidi ya 70, hivyo ufinyu huo ulikuwa ukisababisha msongamano wa abiria.

Amesema watahakikisha wanasimamia vizuri mradi huo ili uweze kukamilika kwa wakati.

“Mkandarasi amepewa mkataba wa mwaka mmoja, lakini yeye mwenyewe ametoa ahadi wakati tunamkabidhi saiti kuwa matarajio yake ni kujenga ndani ya miezi sita, hatarajii kufika mwaka mmoja,”amesema.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *