Upanuzi wa Bandari ya Tanga wapaisha mapato

BANDARI ya Tanga imefanikiwa kukusanya mapato ya Sh bilioni tano katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea Bandari ya Tanga.

Alisema mapato hayo yametokana na kukamilika kwa ujenzi wa gati yenye urefu wa meta 450 katika bandari hiyo, hatua ambayo imesaidia kuongezeka kwa shehena ya meli za mizigo.

“Haya ndio mafanikio ya uwekezaji wa takribani Sh bilioni 29 uliofanywa na serikali katika Bandari ya Tanga ambao umesaidia kuongezeka kwa shehena ya mizigo,” alisema.

Aidha alilitaka Shirika la Reli nchini (TRC) kuhuwisha miundombinu ya reli katika eneo hilo la bandari ili kurahisisha shughuli za uzafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwa njia ya reli.

Alisema kuwa kutokana na bandari hiyo kutokuwa na msongamano, inaweza kupokea meli nyingi za mizigo, hivyo ni vema kuboresha miundombinu ya reli iweze kutumika badala ya kutegemea barabara pekee.

“Niwaagize TRC mpaka mradi wa gati ukikamika kabisa, basi na nyie muwe mmemaliza uwekaji wa miundombinu ya reli katika eneo hili la bandari,” aliagiza.

Naye Mhandisi Mkuu kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) Makao Makuu, Hamis Mrutu alisema kuwa ujenzi wa gati mpya awamu ya pili umekamilika kwa zaidi ya asilimia 98.

9.

Alisema mradi huo unatarajia kukamilika katika muda uliopangwa kwani sasa mradi huo upo katika hatua za umaliziaji pekee.

Naye Kaimu Meneja wa Bandari ya Tanga, Peter Milanzi alisema ndani ya kipindi cha miezi mitatu wameweza kupokea meli kubwa tano ambazo zimebeba zaidi ya shehena ya mizigo tani 130,000.

“Zaidi ya ajira za muda mfupi 100 zimeweza kupatikana kutokana na uingiaji wa meli hizo, hivyo unaona namna ambavyo uwekezaji uliofanywa na serikali ulivyoweza kuleta tija kwa wananchi wetu,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button