Upasuaji JKCI waokoa Sh milioni 70
DAR ES SALAAM; KWA mara ya kwanza nchini Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inawafanyia upasuaji kwa njia ya tundu dogo wagonjwa watano wenye tatizo la kutanuka na kupasuaji mishipa ya damu.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa upasuaji huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dk Peter Kisenge amesema upasuaji huo unagharimu kiasi cha Sh milioni 80 ukifanyika ndani ya nchi na Sh milioni 150 ukifanyika nje ya nchi.
“Kwa mara ya tatu tunavunja rekodi tumefanya matibabu makubwa ya kurekebisha mishipa ya damu ambayo imetanuka na kupasuka hii ni tatizo watu wengi wanapata na kupoteza maisha ghafla na wagonjwa wengi mara nyingi wanapoteza maisha na wanaobaki tunawapeleka India sasa tutaanza kuwahudumia hao wagonjwa.
Dk Kisenge amesema upasuaji huo umefanywa na madaktari wazawa kwa kushirikiana na madaktari kutoka India.
Amesema mgonjwa mmoja tayari ameshafanyiwa upasuaji huku wengine watatu watafanyiwa upasuaji leo na mmoja kesho.
“Ni upasuaji mkubwa Tanzania na Afrka Mashariki na Kati tumevunja rekodi tunampongeza Rais kwa kuwapenda wananchi wake,”ameeleza.
Amebainisha kuwa mishipa kutanuka na kupasuka inasabahishwa na vitu vingi ikiwemo shinikizo la juu la damu ambayo haitibiwi vizuri,uvutaji wa sigara,unywaji pombe uliokithiri na uzito mkubwa.
Dk Kisenge ameeleza kuwa hakuna utafiti uliofanyika ila ni tatizo lipo ambapo wagonjwa 30 wanasubiri matibabu.