DSM; TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), imepokea vifaa tiba, vipandikizi na vifaa vya upasuaji vya kisasa vyenye thamani ya Sh bilioni 3 kutoka jumuiya ya Stant Roch iliyopo nchini Uingereza, ikiwa ni hatua ya ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza.
Uwepo wa vifaa hivyo utaongeza kiwango cha upasuaji kutoka wagonjwa 26 kwa siku kwenda wagonjwa 42 kwa siku.
Aidha MOI sasa inaendelea na kambi ya matibabu iliyoanza Septemba 18 hadi 25 ,2023 ambapo jumla ya wataalamu 18 wakiwemo madaktari 10 na wataalamu vifaa nane kutoka St Roch wanashiriki.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, wakati akipokea vifaa hivyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Dk John Jingu amesema miongoni mwa vifaa vilivyoletwa mgonjwa atafanyiwa upasuaji kwa njia ya matundu hivyo wagonjwa watapata huduma nzuri zaidi.
Pia amesema kambi ya upasuaji ni sehemu nzuri kwa madaktari wachanga, kwani wanajifunza mambo mengi hivyo wanatazamia madaktari wazawa watapata utaalamu kutoka kwa madaktari hao na kuwapongeza kwa fursa hiyo muhimu.
“MOI haitakuwa ile ya mwanzo itabadilika katika siku hizo nane, ambayo mtakaa itakuwa na uzoefu zaidi kutoka kwenu katika nyanja mbalimbali kila mmoja ana nafasi ya kujifunza kutoka kwa mwingine, hivyo nafasi hii italeta matokeo chanya ya muda mrefu kwa jamii yetu, MOI itakuwa kituo cha umahiri katika ukanda huu, hivyo nchi jirani pia watanufaika,”ameeleza.