Upatikanaji maji vijijini wafikia asilimia 64 Singida

UPATIKANAJI wa maji katika vijiji mkoani Singida umeongezeka kutoka asilimia 57 Mwaka 2020 hadi asilimia 64 Februari 2023.

Hayo yalielezwa na Mkuu wa Mkoa huo, Peter Serukamba wakati akizungumzia mafanikio yaliyofikiwa katika Miaka Miwili ya uongozi wa Rais wa Tanzania wa Awamu ya Sita, Dk Samia Suluhu Hassan.

Alisema hatua hiyo imefikisha huduma ya maji kwa wakazi 955,131 katika vijiji tofauti vya mkoani humo.

“Kuanzia 2021 hadi Februari 2023 Ofisi ya RUWASA (Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini) ilipokea jumla ya Shilingi Bilioni 21.758 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji vijijini,” alisema Serukamba.

Alisema ndani ya muda huo, jumla ya miradi 37 ya maji inayotumia mtandao wa bomba ambayo inahudumia wananchi 231 wanaoishi vijijini, imejengwa.

Kwa mujibu wa Serukamba, upatikanaji wa maji katika Mji wa Kiomboi umeongezeka kutoka asilimia 30 hadi asilimia 65, huku katika mji wa Manyoni ukiongezeka kutoka asilimia 65 hadi 73.5 kati ya  mwaka 2020 na Februari mwaka huu.

Wakati huo huo, alisema kupitia Mpango wa Taifa wa Maendeleo Endelevu na Mapambano dhidi ya UVIKO – 19, Januari mwaka huu, mkoa huo umepokea mtambo wa kuchimba visima virefu na kwamba mpaka 28 Februari 2023, visima 11 vilikuwa vimechimbwa wilayani Manyoni na Singida.

Alisema kwa kutumia mtambo huo, maeneo yote yasiyopata maji yatapata, lengo likiwa ifikapo mwaka 2025 upatikanaji wa maji mijini uwe umefikia asilimia 95 na vijijini asilimia 85.

Habari Zifananazo

Back to top button