Upatikanaji wa dawa waimarika Nyang’wale

SERIKALI imefanikiwa kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwenye vituo vya afya wilayani Nyang’hwale mkoani hapa, kutoka asilimia 85 mwaka 2020/21 hadi asilimia 87 mwaka 2021/22.

Takwimu hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Jamuhuri William alipokuwa akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya wilaya kwa Mkuu wa Mkoa, Martin Shigella.

Jamuhuri alisema mbali na hatua hiyo, serikali inaendelea kuhakikisha dawa, vitendanishi na vifaa tiba vinapatikana kwenye vituo tiba vyote ili wananchi wapate huduma bora za afya.

“Wilaya inaendelea na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma ya afya ambapo miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa kwa fedha kutoka serikali kuu, wadau wa maendeleo na nguvu za wananchi,” alisema.

Alisema hadi sasa wilaya ina vituo vya kutolea huduma za afya 24, kati yake vituo 22 ni vya serikali, viwili vya binafsi na halmashauri inaendelea na ujenzi wa vituo saba, ikiwemo zahanati tano. “Kukamilika kwa vituo hivi kutasaidia kuongeza uwepo wa huduma za afya karibu na wananchi na halmashauri itakuwa na jumla ya vituo 28.

Mahitaji ya watumishi wa afya ni 842 na waliopo ni 192,” alisema. Shigella alipongeza mafanikio hayo na kumwagiza Mganga Mkuu wa Wilaya kufuatilia kwa ukaribu upatikanaji dawa kutoka Bohari ya Dawa (MSD).

“Tuendelee kujipanga vizuri tujue kama Nyang’hwale tumepeleka pesa MSD, tumepeleka kiasi gani, na kama dawa tumeletewa, tumeletewa dawa za thamani kiasi gani, na bado tunadai kiasi gani,” aliagiza.

Habari Zifananazo

Back to top button