Upimaji wa ‘mchongo’ sababu U.T.I,

taifodi kutesa wanawake, watoto

TATIZO la maambukizi kwenye njia ya mkojo (Urinary Tract Infection-U.T.I) limekuwa tishio katika jamii hivi sasa kutokana na watu wengi kujihalalishia wana tatizo hilo wanapojisikia kuumwa na upimaji holela.

Pia ugonjwa wa homa ya matumbo (taifodi) nao unatajwa kwa kiasi kikubwa na watu kuwa nao hata kabla hawajapima.

Watu wengi hulinganisha dalili na kuanza kutumia dawa wakijihalalishia kuwa na U.T.I au taifodi na wanapofika kwa daktari hutangulia kueleza wana maradhi hayo kabla ya vipimo.

U.T.I inasababishwa na vijidudu vinavyotoka sehemu ya haja kubwa au mdudu mwingine tofauti kuingia kwenye mfumo wa mkojo. Taifodi ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vya bakteria aina ya salmonella typhi.

Akizungumza na HabariLEO, daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Lilian Mnabwiru, anasema magonjwa hayo mtaani sasa kila anayeumwa akienda hospitali anamwambia daktari anayo.

“Wengi wanakuja wakiwa na magonjwa hayo kabla hawajapimwa na tatizo limekuwa kubwa watu wanatumia dawa za antibiotiki zinasababisha usugu wa vimelea dhidi ya dawa kwa sababu mtu anatibiwa kitu asichonacho.

Anasema U.T.I ni maambukizi kwenye njia ya mkojo ambapo kuna mirija, kibofu na sehemu ya kutokea haja ndogo kwa mwanamke na kwa mwanaume sehemu ya kutokea mbegu ndio ya kutokea haja ndogo. Maeneo hayo ndio yanayoathirika.

Dk Mnabwiru anabainisha maambukizi yanakuwa kwenye mrija au sehemu ya mwisho ambayo haja ndogo inatoka na maumivu yanaanzia kwenye njia hiyo.

Wanawake wanaathirika zaidi

Dk Mnabwiru anasema wengi wanaopata U.T.I ni wanawake na wanafika hospitali kwenye hali ya usugu.

“Jamii inahitaji kuelewa matumizi ya vyoo, mtu akikojoa, mkojo unaruka juu unaweza kuleta maambukizi.”

Anasema kuna tatizo la maabara za mitaani pia ambapo mtu akipimwa anaambiwa ana taifodi au U.T.I wakati hawana uwezo wa kupima magonjwa hayo.

Pempasi zinaathiri watoto kupata U.T.I

Uvaaji wa muda mrefu wa nepi za kisasa (pempasi) unatajwa na wataalamu wa afya kama njia rahisi ya kuambukiza U.T.I kwa watoto hasa wa kike.

Aidha, watoto wa kike wanatajwa kuathirika zaidi hasa wanapokaa na nepi hizo muda mrefu mfano kuanzia asubuhi mpaka jioni au kwa kujaa muda mrefu.

“Mtoto anatakiwa kuvalishwa chupi ili awe huru na ni muhimu tutumie pempasi kwa uangalifu kwani inasababisha madhara akikaa nayo kwa muda mrefu,” anasisitiza Dk Mnabwiru.

Madhara matumizi holela ya dawa

Dk Mnabwiru anasema matumizi holela ya dawa yanasababisha figo kushindwa kufanya kazi na pia inasababisha usugu wa dawa dhidi ya vimelea vya magonjwa. “Dawa zinapokuwa sugu kutibu ni changamoto.”

Unawezaje kupata U.T.I?

Kwa mujibu wa Dk Mnabwiru, mtu anaweza kupata U.T.I wakati wa kujamiiana hasa katika mazingira yasio salama.

Pia anasema mtu anaweza kupata ugonjwa huo wakati akiwekewa mpira wa mkojo kama akiwekewa kwa njia isiyo safi.

Anasema wapo watu wana tatizo la kutomaliza haja ndogo yote hivyo mkojo unaobaki husababisha maambukizi na tatizo hilo linawakumba zaidi watu wazima.

“Wengine watu wazima ile njia ya mkojo inaanza kupungua vitu vinasinyaa kwa homoni za kike kushuka vitu vinavywea hata viungo vya ndani vya mwili vinanywea,” anasema.

Anaeleza pia mazingira mtu anayatumia wakati wa kujisaidia haja kubwa ni sababu. “Wakati wa kujitawadha anaanza nyuma kwenda mbele, hii ni hatari, tunashauri wajisafishe kwenda nyuma.”

Dalili za mtu mwenye U.T.I, taifodi

Anasema dalili za U.T.I ni mtu kupata maumivu anapoanza au kumaliza haja ndogo, kukojoa mara kwa mara wakati mtu anapotoka kushiriki tendo la ndoa katika mazingira yasiyo safi.

Dalili zingine ni kushindwa kuzuia mkojo, kupata maumivu chini ya tumbo, mkojo kutoa harufu. Hatua ya juu mtu anapata dalili za homa, maumivu katika kizazi na kujisikia vibaya.

Kwa taifodi anasema dalili zake zinafanana na malaria. Homa kali, kuharisha, kutokupata haja kubwa, kichefuchefu, kutapika na kupata homa ya kusisimka mwili na maumivu ya misuli na kichwa kuuma.

Namna ya kugundua  

Dk Mnabwiru anasema hatua ya kwanza ya kugundua kama mtu ana ugonjwa husika ni kusikiliza historia yake ya dalili alizoona na kuzifikiria kama zinaweza kuwa ni hilo tatizo.

Anasema daktari baada ya kumsikiliza mgonjwa anakuwa na makisio ya tatizo na ili kuthibitisha, anamwandikia mhusika vipimo.

“Kitaalamu tunatakiwa kujua historia na baadaye vipimo vinafanyika kujua kama kuna maambukizi ya bakteria au mazingira aliyopitia mfano tendo la ndoa kuna wadudu ambao wakienda sehemu ambayo si yao wanapata maambukizi.

“Pengine huyo mtu ametumia dawa za awali lakini hazijamsaidia kuna kipimo cha kujua wadudu gani wako pale, inategemea karudi na shida gani na vipimo vingine vinafanyika hospitali kubwa kuanzia wilaya.

Anasema ili ugonjwa usijirudie hushauriwa kufanya ngono salama, mazingira safi na namna ya kutawadha.

“Kuna wengine wanaambiwa wanywe maji kusafisha njia ya mkojo inasaidia na kutoa dawa sahihi kuna changamoto, kuna mwingine mara ya kwanza anapotibiwa anapewa dawa za gharama kubwa hapa mtoa huduma anaangalia faida zaidi kitu ambacho ni hatari kwa mtumiaji,” anaeleza.

Anasema wagonjwa wenye U.T.I kali hupewa dawa tofauti na wenye U.T.I ya kawaida. Anasema changamoto ni utoaji wa dawa umekuwa holela.

Ushauri kwa jamii

Anashauri endapo mtu atashiriki tendo la ndoa, akojoe haraka na kama kuna maambukizi ya wadudu watasafirishwa kwa mkojo.

Kwa ambao mkojo hauishi, anasema kuna mazoezi wanatakiwa kufanya ili uishe na kwa watu wazima ambao homoni zimepungua kuna mafuta anapatiwa awe nayo.

“Waandishi wa habari waelimishe wananchi, mtu anakuja na taarifa nyingi na tayari amejenga imani ni U.T.I hivyo kumbadilisha inakuwa kazi, wengine wanataka aandikiwe dawa wengine ukimwambia aende kunywa maji anaona daktari hajui kazi ni changamoto,” anasema.

Anasema watu waache kwenda kwenye maabara bubu bali wafike katika vituo vya afya kwa uhakika wa vipimo.

Mwisho

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Angila
Angila
21 days ago

Making every month extra dollars by doing an easy job Online. Last month i have earned and received $18539 from this home based job just by giving this only mine 2 hrs a day. Easy to do work even a child can get this and start making money Online. Get this today by follow instructions……
.
.
.
On This Website……………..> > W­w­w.S­m­a­r­t­c­a­r­e­e­r­1.c­o­m

Back to top button
1
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x