Upungufu wa madawati kushughulikiwa Manyara

MKUU wa Mkoa wa Manyara, Qieen Sendiga amezindua kampeni maalumu ya kukabiliana na upungufu wa meza na viti 4,664 na Madawati 28,336 katika Mkoa wa Manyara na kampeni hiyo inajulikana kwa jina la ‘’Mpe Maua Atabasamu Asome Kifalme ‘’ na kuwataka wadau wa maendeleo mkoani Manyara kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha elimu.

Sendiga alisema hayo wakati akizindua kampeni hiyo kimkoa katika mji wa Mirerani wilayani Simanjiro katika Shule ya Msingi Mirerani na kuwataka wawekezaji wa sekta zote Manyara, wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa sekta ya madini ya Tanzanite na taasisi za dini, umma na binafsi kumuunga mkono katika jitihada za kutaka mwanafunzi kusoma akiwa amekaa kwenye kiti.

Alisema Rais Samia Suluhu Hassan ameleta katika Mkoa wa Manyara Sh bilioni 94 katika sekta ya elimu pekee yake hivyo wadau wa maendeleo na elimu wanapaswa kumuunga mkono Rais katika jitihada zake za kuboresha elimu mkoani Manyara kwa kuchangia madawati,viti na meza.

Sendiga alisema wadau mkoani Manyara wanawajibu wa kuunga mkono jitihada za Rais ikiwa ni pamoja na kukutana na kupanga namna gani wanaweza kutatua changamoto ya upungufu wa madawati kwa kuchangia fedha kwa kila mmoja kujitoa yeye binafsi ama kampuni yake na sio vinginevyo.

Alisema Mkoa wa Manyara unakila sifa ikiwemo madini ya Tanzanite na Michezo hivyo ni wajibu wa kila mdau wa mendeleo Manyara popote alipo kuhakikisha analitimiza hilo kwa maendeleo ya watu wa Mkoa wa Manyara.

Mkuu huyo wa Mkoa alishukuru kampuni ya madini ya Franone chini ya Ukurugenzi wa Onesmo Mbise na Francis Matunda kwa kumwanzishia kampeni yake kwa kuchangia madawati 100 yenye thamani ya shilingi milioni 8 na wadau wengine wa Maendeleo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Simanjiro Kiria Laizer kuchangia madawati 42 yenye thamani ya Sh milioni 3.

Sendiga aliwataka wadau wengine wa maendeleo Mkoani Manyara ,Wafanyabiashara wa sekta mbalimbali ,wawekezaji wa madini na utalii kuiga mfano wa Franone katika kurudisha faida kwa jamii bila ya kusukumwa.

‘’Kampeni hii nimeizindua kwa Mkoa wa Manyara hapa Mirerani ili kuhakikisha kila mwanafunzi wanakaa katika viti kupata elimu na Franone wameshaanza na wametuanzishia hivyo tumunge mkono’’alisema Sendiga

Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro,Suleman Serera alisema kuwa katika wilaya hiyo Sh bilioni 21 zimeletwa kwa ajili ya elimu hivyo basi wadau wa Maendeleo wanapaswa kumuunga mkono Rais kwa kutatua upungufu wa madawati katika wilaya hiyo na Mkoa kwa ujumla.

Alisema na kuwaasa wadau wa elimu katika maendeleo hakuna siasa na wenye kutaka kuchanganya siasa na maendeleo hawapaswi kupewa nafasi hivyo kinachongaliwa kwa sasa ni kukabiliana na upungufu wa madawati Kimkoa na siasa zitakuwa wakati ukifika.

Serera alisema mambo ya siala katika maendeleo Wilaya Simanjiro hayana nafasi na kuwataka wadau kumuunga mkono Mkuu wa Mkoa katika kampeni yake ya kukabiliana na upungufu wa madawati Mkoani Manyara.

Naye Meneja wa Franone,Vitus Ndaikize alisema kuwa kampuni ilifikwa baada ya kusikia kuwa shule Kongwe ya Msingi Mirerani yenye wanafunzi 1,276 ikiwa na upungufu wa madawati na wakurugenzi waliamua kujitoa na kutoa msaada huo ikiwa ni jitihada za kumuunga mkono Rais katika kuboresha elimu,afya,maji na barabara Mkoani Manyara kwani ni wajibu wao kurudisha faida kwa jamii.

Ndaikize alisema sio mara ya kwanza kutoa msaada katika kuunga mkono jitihada za serikali kwani wameshafanya hivyo mara kwa mara wao wenyewe na pindi wanapohitajika kufanya hivyo wanafanya bila ya wasiwasi.

Naye Mwenyekiti wa CCM,Kiria Laizer alisema kuwa wadau wa elimu na maendeleo Simanjiro wanapaswa kujitoa katika kukabiliana na upungufu wa madawati Simanjiro na Mkoa kwa ujumla kwani wanafunzi wanaosoma waweze kupata elimu bora zaidi.

Habari Zifananazo

Back to top button