KAMPUNI kubwa ya nishati ya Urusi, Gazprom imetangaza Ijumaa kwamba usafirishaji wa gesi asilia hadi Umoja wa Ulaya kupitia bomba la Nord Stream 1 utasitishwa kuanzia Agosti 31 hadi Septemba 2 kwa matengenezo.
“Mnamo Agosti 31, kitengo pekee cha kujazia gesi cha Trent 60 kinachofanya kazi kitafungwa kwa siku tatu kwa ajili ya matengenezo,” kampuni hiyo ilisema, ikibainisha kuwa ukarabati wote utafanywa kwa pamoja na wataalamu kutoka kwa mtengenezaji wa Ujerumani, Siemens.
Gazprom iliongeza kuwa “Baada ya kukamilika kwa kazi na kutokuwepo kwa hitilafu za kiufundi za kitengo, usafirishaji wa gesi utarejeshwa kwa kiwango cha mita za ujazo milioni 33 kwa siku,” ikiwa ni pamoja na takriban asilimia 20 ya uwezo kamili wa bomba.
Kitengo hicho ndicho cha mwisho kati ya mitambo sita ya bomba hilo ambayo ilikuwa ikifanya kazi, huku nyingine zikihitaji kufanyiwa marekebisho. Moja ya turbines kwa sasa imekwama nchini Ujerumani kutokana na vikwazo, baada ya kurudi kutoka kwa kazi za ukarabati nchini Canada.