UMOJA wa Falme za Kiarabu umeongeza ununuzi wake wa mafuta ghafi ya Urusi licha ya ongezeko la shinikizo kutoka kwa Marekani na washirika wake wa Magharibi kuzuia biashara na Moscow, Reuters iliripoti Jumanne, ikinukuu data na vyanzo vya kufuatilia meli.
Takwimu zinaonyesha kuwa takriban mapipa milioni 1.5 ya mafuta yasiyosafishwa ya Urusi yamesafirishwa hadi katika taifa hilo la Ghuba tangu Novemba, huku kiasi cha jumla kikiwa kimeongezeka tangu mapema mwaka 2022. Mizigo ya hivi karibuni zaidi ya mafuta ghafi ya Urals ya Urusi imeripotiwa kufika katika kitovu cha mafuta cha Fujairah mapema mwezi huu.
Kulingana na kampuni ya uchanganuzi wa nishati ya Kpler, usafirishaji wa kwanza ulifanyika mwaka wa 2019 lakini usafirishaji uliongezeka baada ya Aprili 2022, na kusitishwa kati ya Julai na Oktoba 2022.
Data kutoka kwa jukwaa la uchambuzi wa kifedha la Refinitiv Eikon inaonyesha kuwa usafirishaji wa kwanza wa Urusi kwenda UAE ulikuwa 2022, na kuongezeka kwa Aprili.