Urusi yapeleka wakufunzi 100 wa kijeshi Niger

NIGER; WAKUFUNZI wa kijeshi wa Urusi wamewasili Niger wakiwa na mfumo wa ulinzi wa anga na vifaa vingine kama sehemu ya kuimarisha uhusiano wa usalama wa taifa hilo la Afrika Magharibi na Moscow.

Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kwamba serikali ya kijeshi ya Niger ilikubali mwezi Januari kuongeza ushirikiano wa kijeshi na Urusi, baada ya kuwafukuza wanajeshi wa Ufaransa waliokuwa wakisaidia kupambana na waasi wenye silaha katika mataifa kadhaa.

Mtangazaji wa Tele Sahel alionyesha ndege ya uchukuzi ya Urusi ilipokuwa ikiwasili katika uwanja wa ndege wa Niamey ambapo wakufunzi wa kijeshi kutoka Wizara ya Ulinzi ya Urusi walikuwa wametua katika mji mkuu wa Niger wakiwa na vifaa vya mfumo wa anga.

Urusi itasaidia kuweka mfumo wa ulinzi wa anga ili kuhakikisha udhibiti kamili wa anga ya Niger.

Televisheni ya serikali ya Niger iliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook kwamba wakufunzi100 wa kijeshi wa Urusi wamewasili Niamey.

Hata hivyo licha ya jeshi hilo kutua Nigera hakukuwa na maoni kutoka kwa Urusi, ambayo imekuwa ikitaka kuongeza ushawishi wake kwa nchi za bara la Afrika, ikijitangaza kama nchi rafiki isiyo na misingi ya kikoloni katika bara hilo.

Niger ilikuwa mshirika wa mstari wa mbele wa nchi za Magharibi katika kupambana na wapiganaji wenye silaha huko Sahel lakini imegeukia Urusi tangu mapinduzi ya Julai iliyopita yaliyompindua Rais mteule Mohamed Bazoum.

Mwezi Machi, Niger iliamua kubatilisha makubaliano yake ya kijeshi na Marekani ambayo yaliruhusu wafanyakazi wa Pentagon kufanya kazi kwenye ardhi yake kwa vituo viwili ikiwa ni pamoja na kambi ya ndege zisizo na rubani ilizojenga kwa gharama ya zaidi ya $100m.

Marekani bado inadumisha takriban wanajeshi 1,000 nchini Niger, lakini mienendo yao imekuwa ikipungua tangu mapinduzi hayo.

Habari Zifananazo

Back to top button