KAMPUNI kubwa ya nishati inayomilikiwa na serikali ya Urusi, Gazprom ilithibitisha Jumanne kuwa imesitisha usambazaji wa gesi kwa kampuni ya huduma ya Ufaransa ya Engie. Kampuni hiyo yenye makao yake mjini Paris imeshindwa kulipia gharama za usambazaji wa gesi ya mwezi Julai, Gazprom ilisema.
Gazprom iliarifu Engie kwamba itasitisha utoaji wa gesi kuanzia Septemba 1 hadi wakati itakapopata malipo kamili ya gesi ambayo tayari imetolewa, kampuni hiyo kubwa ya nishati Urusi ilisema katika taarifa. Pia ilibainisha kuwa upande wa Ufaransa ulishindwa kufanya malipo hayo kufikia Jumanne jioni, na kufanya Gazprom kusitisha usambazaji wa gesi kwa mujibu wa sheria za Urusi.
Mapema siku hiyo, Engie alionya kwamba Gazprom iliiarifu “kupunguzwa kwa usambazaji wa gesi” na ikataja “kutokubaliana kati ya wahusika juu ya utumiaji wa mikataba kadhaa,” mtandao wa Bloomberg uliripoti. Haikutoa maelezo yoyote kuhusu hali ya kutokubaliana na haikufafanua kiwango cha vikwazo vya utoaji.
Waziri wa Nishati wa Ufaransa Agnes Pannier-Runacher aliishutumu Moscow kwa kutumia mauzo yake ya gesi kama silaha siku ya Jumanne. Pia alisema kwamba Ufaransa “lazima ijiandae kwa hali mbaya zaidi.” Kauli yake ilitolewa kabla ya tangazo la Gazprom.