USAID, serikali wang’arisha kilimo cha viungo Tanga

NILIANZA kilimo mwaka 2008 nikiwa darasa la sita nikimfuata mama yangu shambani na nilipofika darasa la saba mwaka 2010 nilianza kumiliki shamba la robo eka baada ya mama kuniachia ikiwa na migomba sita.

“Nilianza kupanda hiliki,” anasimulia Andrea Ndale (29), mkazi wa Kijiji cha Kizerui kilichopo Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Kijiji cha Kizerui kinapatikana katikati ya Ushoroba wa hifadhi ya misitu ya asili ya Amani na Nilo na kina watu 1,765. Eneo la kilimo hai ni ekari 785.6 huku wakulima wakijihusisha na kilimo cha viungo kama hiliki, karafuu, mdalasini na pilipili manga.

Akiwa mmoja wa vijana wakulima katika kijiji hicho, Ndale ambaye ni baba wa watoto wawili sasa anasema aliishia kidato cha pili kutokana na mama yake kushindwa kulipia ada ya shule.

“Mfumo wa kilimo wa mwanzo haukuwa mzuri kwani wakulima walikuwa wanauza mazao yakiwa shambani, maarufu makalaza kwa bei ndogo ya kinyonyaji hivyo faida ya kilimo ilikuwa haionekani hapa kijijini,” anasimulia.

Anasema hivi sasa wamepata elimu kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wa Tuhifadhi Maliasili hatua iliyowaongezea ufahamu wa kulima kilimo chenye tija zaidi.

“Matarajio yangu ni makubwa kwani mashamba nimeongeza ekari nne na ekari moja ya hiliki ambayo nachuma ndoo 45 na ekari moja na nusu yenye mikarafuu 80 japo sijapanda kisasa kwa sababu elimu ilikuja hivi karibuni,” anafafanua.

Ndale anasema si kilimo tu pia elimu hiyo imewasaidia kuunda vikundi vya kuweka akiba na kukopesha hatua inayowasaidia wasiuze mazao shambani.

“Ndani ya miaka mitatu nitakuwa na mafanikio kuanzia mwaka 2026 kwani natarajia kumiliki gari na familia yangu iishi maisha mazuri. Tunataka tuishi kama mjini, watoto wangu wasome shule nzuri pia niwe mfanyabiashara mkubwa wa viungo,” anaeleza Ndale.

Anawashauri vijana hususani wa vijiweni wanaofanya vitendo visivyofaa, warudi kulima kwani sasa kilimo kinalipa. Yeye amepata kilogramu 15 za hiliki na kilo moja ameuza Sh 18,000 ambapo pia mwaka huo kulikuwa na uchache wa mvua kwani angepata kilo 100 kama mvua zingekuwa nyingi.

“Nawashauri jamii wajiunge kwenye vikundi vya kuweka na kukopa na hawatakuwa kule kwenye kuchukua ‘makalaza’. Watanufaika kwani tutakopeshana wenyewe kwa wenyewe na tunatarajia kuitisha mkutano wa kijiji kutoa elimu kwa wote kwa vitendo na kuwashawishi,” anasisitiza.

Hivi sasa vijiji saba vilivyopo katika ushoroba wa Hifadhi ya Misitu ya Amani na Nilo vinanufaika na Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili na kutekelezwa na Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG).

Kizerui ni miongoni mwa vijiji hivyo na vingine ni Zirai, Antakae, IBC Msasa, Shamba Ngeda, Kwendimu na Magoda.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Kizerui, Andrew Kingazi anasema kupitia mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili wamekuwa wakipata mafunzo ya utunzaji mazingira na kilimo hai na kufanya wakulima kuacha kutumia kemikali na kujua kuweka akiba kupitia vikoba.

“Faida ya kilimo hai ni kubwa na mazao yana soko kubwa. Wananchi baada ya kupewa elimu ya kilimo hai wana mwamko mkubwa wa kilimo lakini changamoto ni soko la uhakika ambapo kwa mwaka huu tumejadili kukutana na wadau kuzungumzia kuingia katika soko la dunia,” anadokeza.

Ofisa Misitu wa Wilaya ya Muheza, Obadia Msemo anasema kwa sasa wana mashirika yanayofanya kazi na serikali katika maeneo ya utunzaji wa rasilimali za misitu, vyanzo vya maji na matumizi bora ya ardhi ambapo mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umefanikiwa kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Msemo anasema wamefanikiwa kuwajengea uwezo serikali za vijiji kwa kuwafundisha namna ya matumizi endelevu ya rasilimali hizo.

Anasema faida yake ni jamii kusimamia ardhi yao na kufanya shughuli zao kwa kufuata utaratibu katika maeneo ya misitu na wameweka sheria za namna ya kuitunza, kuisimamia na kuitumia.

Anafafanua kuwa Mradi wa Tuhifadhi Maliasili umewasaidia hasa katika vile vijiji vilivyoko moja kwa moja kwenye ushoroba wa Amani Nilo inayotambulika kama Derema.

Anasema mradi huo umeongeza uandaaji mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo kuna hatua sita. Anasema miradi mingi ya nyuma waliishia hatua nne hadi tano lakini hatua ya mwisho ya upimaji na kutoa hatimiliki ilikuwa haijafikiwa.

Anasema hatua hiyo imesaidia kuondoa migogoro ya mipaka baina ya vijiji na vijiji kwani kupitia ofisi ya ardhi wamepanga matumizi ya ardhi.

Naye Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza, Oyange Mbwambo anafafanua kuwa mradi umewasaidia wakulima kutunza mazingira na kuwa endelevu hali inayofanya uzalishaji wa viungo usirudi nyuma na maeneo yale ndio vyanzo vya maji vinapatikana kusambaza maji Jiji la Tanga.

“Tuna vikundi vya wakulima zaidi ya 22 katika kata za Zirai na Misalai na kwa kujali shughuli zao tumeongea na wadau tukapata shirika wakatengeneza chama kimoja cha ushirika kinaitwa Zimisa na wamewasaidia kuwapa elimu ya kilimo bora, usindikaji, ujasiriamali na wamewajengea ghala kama chama watakusanya mazao yao na wamewawekea mashine ya kukaushia,” anafafanua Mbwambo.

Mkazi wa Kijiji cha Kizerui, Stephano Diwa anasema anatamani waanzishe vyama vya ushirika ili wapate bei nzuri ya mazao na kuondoa changamoto ya ulanguzi inayowakabili kwa sasa.

Kwa sasa anaeleza wanauza mazao hayo kila mtu na bei yake kwa sababu yakuwepo walanguzi.

“Mfano kipindi cha nyuma walikuwa wananunua kilo moja ya karafuu kwa shilingi 9,000 hadi 10,000 na wanauza kwa shilingi 15,000 hadi 20,000 na kupata faida wao lakini sisi hatufaidiki na kilimo hicho hivyo tunatumia nguvu nyingi bila faida,” anasimulia.

Mkazi mwingine, Selina Kusaga anaeleza wanapata changamoto kuuza mazao kwa bei ya chini ambayo haina tija kwao na wanazalisha mazao hayo mara moja kwa mwaka.

“Tunaendelea kuwa masikini na wengine wanatajirika kupitia sisi. Hili linatuumiza sana sisi wakulima wa hapa Kizerui na mazao yetu yanasoko zuri tu duniani,” anasema.

Mkazi wa Kijiji cha Antakae, Bertha Maguluko anabainisha changamoto ya uchafuzi wa ubora wa karafuu kwa kuchanganywa na vikonyo hali inayosababisha bei ya karafuu ya Tanzania kuonekana kutokuwa na ubora.

“Sisi wakulima tunatenga vizuri karafuu zetu lakini wafanyabiashara wanakuja kuchanganya na vikonyo hali inayosababisha karafuu yetu ionekane kuwa haina ubora kitu ambacho si sahihi kama kukiwa na sehemu moja ya kuuza itakuwa ahueni,” anasema akisisitiza umuhimu wa chama cha ushirika.

 

Habari Zifananazo

Back to top button