Usajili wa Kisinda zogo

KLABU ya Yanga italazimika kusubiri mpaka Desemba ili kumtumia winga wake mpya Tuisila Kisinda iliyemsajili siku ya mwisho ya dirisha la usajili Agosti 31.

Hiyo inatokana na mchezaji huyo kukosa leseni kutokana na klabu hiyo kutimiza idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa kama kanuni za Shirikisho la soka Tanzania TFF zinavyoeleza.

Yanga ilitangaza kumsajili Kisinda siku ya mwisho ya pazia la usajili na ililituma jina lake kwenye orodha ya wachezaji wake lakini TFF ilishindwa kumuidhinisha kutokana na matakwa ya kanuni yanayotaka wachezaji 12 wa kigeni na ambayo Yanga walishakamilisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TFF kwa vyombo vya habari jana,  usajili wa wachezaji wa kigeni, hasa kwa klabu ambazo zinashiriki mashindano ya kimataifa ulishapitishwa na Kamati ya sheria na hadhi za wachezaji ya TFF.

Kanuni ya 62(1) ya Ligi Kuu toleo la 2022, klabu inaruhusiwa kusajili wachezaji wa kigeni wasiozidi 12 hivyo, klabu kutaka au kujaribu kusajili wachezaji zaidi ya idadi hiyo ni kwenda kinyume na kanuni husika.

Inaelezwa kuwa uongozi wa Yanga, ulikuwa na mpango wa kulikata jina la mchezaji mmoja, Lazarous Kambole kutokana na kuwa majeruhi ya muda mrefu, lakini ikashindikana kwa vile Kamati ilishapitisha usajili muda mrefu na leseni zilishatoka.

Gazeti hili lilimtafuta Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh kuzungumzia suala hilo ambapo alisema wanasubiri taarifa ya kukutana kiofisi kulijadili hilo.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button