Ushirikiano Serikali, viongozi wa dini kuendelezwa

KAGERA: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, amesema Rais Samia Suluhu Hassan  ataendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki na madhehebu mengine ili kwa pamoja walete maendeleo nchini.

Dk Doto Biteko,ameyasema hayo Januari 27 alipomwakilisha Rais, Samia katika Sherehe za kuwekwa wakfu na kusimikwa kwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Bukoba, Mhashamu Jovitus Mwijage ikiwa ni tukio la kihistoria kutokana na kupita takriban miaka 50 kutoka kufanyika sherehe kama hiyo ya uwekaji wa wakfu.

Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Kaitaba wilayani Bukoba Mkoa wa Kagera, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.

Amesema Rais anatambua kuwa bado kuna changamoto mbalimbali nchini ambazo serikali inafanya kila jitihada ili kuzindoa lakini hili litafanyika kwa ufanisi endapo hakutakuwa na mgawanyiko nchini kama ambavyo ilivyo sasa.

Pia,ameeleza, Serikali inatambua kuwa kuna tofauti nyingi nchini ikiwemo za makabila na madhehebu lakini tunu inayounganisha watu wote ni haki, uhuru, umoja na amani ambayo Mwenyezi Mungu ameijalia nchi.

“Rais anatambua kutofautiana ikiwemo katika  mawazo  lakini kama mnavyojua kuwa amekuwa ni muumini wa maridhiano kwani anayaishi na anatoa nafasi kwa kila mmoja kutoa mawazo yake bila kubughudhiwa.” Amesema Dk Biteko

Dk Biteko amemtakia kila la heri Askofu Mwijage katika majukumu yake mapya kwenye kanisa na malezi ya jamii kwa ujumla na kueleza kuwa Serikali inatambua umuhimu wa  imani kuwa ni kiini cha ustaarabu na uungwana miongoni mwa jamii.

Ameongeza kuwa, kuwekwa wakfu kwa Askofu Mwijage kunatoa mafundisho mengi ikiwemo kutotanguliza hofu pale kunapotokea majukumu mapya kutokana na Askofu huyo kuwa tayari kutumikia  majukumu yake  bila kuweka vikwazo mbele na kwamba hili ni somo kwa wananchi wengine kuwa tayari kutekeleza majukumu bila kutanguliza vikwazo.

Wakati huohuo, Dk Biteko amempongeza aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Mhashamu Askofu Methodious Kilaini ambaye leo ametangaza kustaafu rasmi na kumueleza kuwa, Serikali inatambua mchango wake na kwamba asisite kutoa mawazo  yake katika kujenga nchi na ustawi wa jamii.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwasa amesema kuwa,  Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa Kanisa Katoliki mkoani humo nia ikiwa ni kuchagiza maendeleo na amani mkoani Kagera.

 

Habari Zifananazo

Back to top button