DODOMA; USHIRIKIANO kati ya Shirika la Viwango nchini (TBS) na lile linalosimamia viwango Zanzibar (ZBS), umeleta matokeo chanya kutatua changamoto za wajasiriamali, wakiwemo kutoka Zanzibar. Bunge limeelezwa.
Naibu Waziri Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, ametoa maelezo hayo bungeni leo Juni 5, 2024 alipokuwa akijibu swali la Mbunge Ameir Abdallah Ameir (Baraza la Wawakilishi), aliyetaka kujua kwa kiasi gani ushirikiano kati ya TBS na ZBS unaleta matokeo chanya na kusaidia kutatua changamoto za wajasiriamali hususani kutoka Zanzibar.
“Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa na mashirikiano na taasisi ya Viwango ya Zanzibar (ZBS) kupitia Hati ya Makubaliano (Memorundum of Understanding – MoU) ya zaidi ya miaka tisa (9) sasa.
“Mheshimiwa Spika, ushirikiano huu kati ya TBS na ZBS unaendelea kuleta matokeo chanya kwa kutatua changamoto za wajasiriamali wakiwemo kutoka Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kutekeleza mifumo ya uandishi wa viwango, usimamizi wa ubora, upimaji na ugezi, na hivyo kusaidia wajasiriamali kuzalisha bidhaa bora na zenye viwango vya kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi,” amesema.