Ushirikina, tiba mbadala zinavyogharimu maisha ya watu

OKTOBA 13, 2022, HabariLEO ilipita katika Taasisi ya Ocean Road (ORCI) na kushuhudia wagonjwa wakiendelea na matibabu.

Baadhi walikuwa waliowahi matibabu ugonjwa ukiwa bado katika hali ya chini na wengine wakiwa wamechelewa na ugonjwa ulikuwa juu.

Nje ya ukuta wa jengo hilo watu wawili walikuwa wakitoka hospitalini hapo. Walionekana kuwa wanatoka kupata matibabu na kurudi nyumbani.

Niliwasogelea ili kuzungumza nao. Nikajitambulisha. Mmoja akasema anaitwa Happy John na mwingine Ester.

Tulikaa sehemu rafiki nami nikawauliza sababu ya wao kuwa pale hospitali.

Happy akajibu: “Nimemleta ndugu yangu kupata matibabu kwani anaumwa saratani.”

Nikamtazama Ester aliyeonekana kuwa mgonjwa. Nikamuuliza aligundulika lini kuwa na ugonjwa.

Akajibu kuwa ni mwaka 2020 baada ya kuanza kuona dalili. Hata hivyo, anasema alichelewa kufika hospitali kutokana na matumizi ya dawa asili.

Ester Dahayo (41) anasema alianza kuona majimaji yenye harufu ukeni na baadaye kutokwa damu baada ya kujamiiana.

Hata hivyo, anasema kutokana na uelewa mdogo, alianza kwenda kwa waganga wa kienyeji kupatiwa matibabu.

“Mimi nimeolewa mke wa pili na kwa sababu huwa tuna ugomvi na mke mkubwa, nilivyoona damu ikinitoka ukeni nilijua moja kwa moja kuwa kaniroga hivyo nikaanza kwenda kwa waganga ili wanisaidie kupona,” anasimulia.

Anasema baada ya kupata matibabu hali yake iliendelea kuwa mbaya na dawa za asili hazikumsaidia hivyo akaamua kwenda hospitali ya mkoa na kupewa rufaa kwenda ORCI (Ocean Road).

Ester anayeendelea kupata matibabu, anawashauri watu kupima afya zao mara kwa mara ili wanapogundulika kuwa na tatizo, waanze mapema kupata matibabu.

WANAOCHELEWA NI WENGI

Ester ni miongoni mwa wagonjwa wengi wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani, magonjwa ya moyo na mishipa ya fahamu, kisukari na magonjwa sugu ya mfumo wa hewa wanaochelewa kufika vituo vya afya kupata matibabu.

Mkurugenzi ORCI, Dk Julius Mwaisalage, anasema takribani asilimia 75 ya wagonjwa wa saratani wanafika wakiwa wamechelewa na wapo katika hatua ya tatu au ya nne ya ugonjwa.

“Hapo wanakuwa wamechelewa, lakini wakiwahi katika hatua ya kwanza au ya pili, ugonjwa unatibika,” anasisitiza.

Mratibu wa Elimu na Kinga ya Saratani kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, Kidaya Christian, anasema wagonjwa wa saratani wanaofika katika hatua ya kwanza na ya pili ni asilimia 40 huku asilimia 60 wanafika katika hatua ya tatu na nne.

“Matibabu kwa mgonjwa kama huyo yanakuwa mengi, kubwa zaidi ni elimu watu wengi hawajui ukweli kuwa, wakiwahi hospitalini watapona; bado wanachukulia mazoea ndio maana unakuta mwanamke anatoka damu kwenye njia ya uzazi isiyo ya kawaida, anapuuzia na kufikiri itaisha au hata kufikiria ushirikina.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge, anasema zipo tafiti ndogondogo zilizofanyika mkoani Arusha.

Kati ya watu 947 waliopimwa, asilimia 20 walikuwa na shinikizo la juu la damu.

“Tuliwauliza kama waliwahi kwenda hospitalini hata kwa ajili ya kuangalia afya zao… Karibu asilimia 30 ya hao wagonjwa walisema hawajawahi kwenda kupima,” alisema.

Anaongeza: “Ukichukua huo utafiti, inaonesha kuna asilimia kubwa tu ya watu ambao hawaendi kuchunguza afya zao, lakini pia, asilimia kubwa ya wagonjwa wanaopenda kufika hospitalini ni wanawake. Kati ya hao 947, asilimia 94 ya akinamama walionesha wameshawahi kwenda hospitali tofauti na wanaume.

Dk Kisenge anasema wagonjwa wengi hasa wa shinikizo la damu wanafika misuli ya moyo ikiwa tayari imeshatanuka na wengine moyo unaanza kushindwa kufanya kazi kwa sababu wameishi na tatizo la moyo kwa muda mrefu bila matibabu.

“Wanakuja kwetu dalili zimeshaanza kuonekana kama kuchoka, miguu kuvimba na tayari wameshapata madhara,” anasema.

Daktari Bingwa wa Ugonjwa wa Kisukari, Profesa Andrew Swai, anasema miongoni mwa changamoto za ugonjwa wa kisukari ni kutokuonesha dalili mapema na hata dalili zinapoonekana, huwa ugonjwa umeshafikia hatua ya juu.

“Wakati sukari imepanda na kuwa ya juu sana na wakati huo sukari inaanza kuwa nyingi kwenye mkojo na figo inashindwa kuchuja,” alisema.

Anafafanua: “Kwa kawaida figo zinachuja vitu vyote kwenye damu; vile vizuri inavirudisha na vibaya vinatoka sasa ukifikia sukari iko juu figo inashindwa kurudisha kwani mtu ukimwona ana sukari kwenye mkojo ni hatua ya juu sana.”

Anasema dalili ya kukojoa mara kwa mara, inaweza kuharibu viungo vya mwili kama ini, macho na maeneo mengine.

“Watu wengi wanakuja wakiwa na kisukari baada ya miaka mitano hadi 10 bila kuwa na dalili, lakini wakati huo, macho yameharibika, mishipa ya damu imeharibika…”

 

TAKWIMU ZIKOJE?

Magonjwa yasiyoambukiza ni magonjwa ambayo vimelea vyake havisambazwi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), mwaka 2016 vifo milioni 42 sawa na asilimia 27 vilitokana na magonjwa hayo.

Kwa Tanzania inakadiriwa kuwa magonjwa haya yanasababisha vifo kwa asilimia 27.

Utafiti wa mwaka 2012 ulionesha kuwa, kwa kila watu 100 wenye miaka 25 na kuendelea, watu tisa wana kisukari, watu 26 wana shinikizo la damu na watu 25 wana mafuta yaliyozidi kwenye damu huku watu 34 wakiwa na uzito uliozidi.

Ikilinganishwa na utafiti wa mwaka 1986/1987, ugonjwa umeendelea kuongezeka kwa kasi.

Katika miaka hiyo ilionesha kuwa kati ya watu 100 ni mtu mmoja alikuwa na kisukari na watu watano tu kati ya 100 walikuwa na shinikizo la damu.

 

MZIZI WA KUCHELEWA HUU HAPA

Matumizi ya tiba asili na imani za kishirikina ni mambo yanayotajwa kuwa miongoni mwa sababu kubwa za wagonjwa kuchelewa kufika katika vituo vya afya au hata kukimbia matibabu hospitalini.

Sababu nyingine zilizoainishwa ni jamii kutokuwa na utaratibu wa kuchunguza afya mara kwa mara na uelewa mdogo kuhusu magonjwa yasiyoambukiza kama  shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kisukari, saratani na magonjwa sugu ya mfumo wa fahamu.

Wataalamu wa afya wanasema tabia hizo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu wengi.

Kidaya anasema matumizi ya dawa asili ni tatizo kubwa kwa wagonjwa kwa kuwa yanachelewesha wagonjwa kupata matibabu sahihi.

Anasema: “Wengine wanaenda kwa waganga wa kienyeji wakiamini kuwa wanarogwa kwa hiyo wanatumia muda mwingi kwenda kujiagua huko na baada ya kushindwa, ndio wanakuja hospitalini.”

Naye Dk Kisenge anasema tatizo ni watu kutokuwa na mwamko wa kupima afya kwa hiari hata kama hawaumwi.

Profesa Swai yeye anasema tatizo lingine ni watu kutafuta dawa mbadala kutokana na sababu za kishirikina au gharama za matibabu ya hospitali kuwa kubwa.

“Sasa waganga wengi hawana tiba ya kweli ya kusaidia wanapoteza muda wanaposhindwa huko ndio wanakuja hospitali, wanapoteza muda kwa sababu ya kutumia dawa asilia na kupokea ushauri kutoka kwa watu mbalimbali,” alieleza.

Anashauri watu kupima afya zao mara kwa mara hasa presha na kisukari kwa sababu hazioneshi dalili.

 

WAHUDUMU WA AFYA WANACHANGIA

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Watoto katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Fransis Furia, anasema wahudumu wa afya pia wamekuwa chanzo cha wagonjwa kutopata matibabu sahihi kwa wakati.

“Uwezo wa watoa huduma wa kutambua magonjwa hayo ni mdogo na watoa huduma wa afya wanawachelewesha, lakini si hao tu na watu pia wanachelewa kwa sababu wanapelekwa wakaombewe au kwenye tiba mbadala,” anasema.

Anasema hata wanaowahi kwenda hospitali, baadhi huangukia katika changamoto ya kuchelewa kwa kuwa wengine wanapata matibabu ya magonjwa mengine kwa kuwa magonjwa hayo yanafanana.

“Mfano, saratani inafanana na kifua kikuu kwa hiyo wanampa dawa za kifua kikuu kwa muda mrefu hali inayosababisha kushindwa kupata matibabu sahihi ya saratani kwa wakati,” anasema.

 

NINI KIFANYIKE?

Profesa Furia anasema: “Jamii na wataalamu wa afya wanatakiwa kupewa elimu na kujengewa uwezo wa kuwahi kuwatambua kwa sababu wakimgundua mapema, watampeleka kwenye huduma sahihi moja kwa moja.”

Anasema sababu za magonjwa hayo yasiyo ya kuambukiza ni mitindo mbaya wa maisha ikiwemo ulaji mbaya na kutokushughulisha mwili.

Anashauri kuzingatia ulaji unaofaa wa mlo kamili na kufanya mazoezi.

Mkurugenzi wa Shirika la Afya Afrika Tawi la Tanzania (AMREF TZ), Dk Florenc Temu anashauri jamii akisema: “Watu wawe na tabia ya kuchunguza afya, tabia ya kusoma, kuishi maisha ambayo hayapelekei uwezekano wa kupata magonjwa na kuchunguza afya mara kwa mara na kupata ushauri wa kitaalamu.”

Kuhusu serikali, anasema watoa huduma wawe na vifaa vya uchunguzi katika hospitali zote kuanzia ngazi ya zahanati hadi ngazi za juu ili watu wasiende hospitali kwa sababu tu wanaumwa, bali waende kwa sababu wanachunguza afya zao.”

Habari Zifananazo

Back to top button