Usimamizi mradi wa mazingira wamchefua DC Tanganyika

MKUU wa Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi, Onesmo Buswelu, ameeleza kutoridhishwa na usimamizi wa mradi wa mazingira unaotekelezwa wilayani humo kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais wenye thamani ya Sh milioni 156.

DC Buswelu ameliambia Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Tanganyika kuwa, fedha hizo zimetolewa kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kutunza mazingira hususani katika chanzo cha mto Katuma kinachopeleka maji hadi Bwawa la Nyerere, lakini hadi sasa zaidi ya shilingi milioni 20 hazijulikani zilipo, huku uharibifu ndani ya mto huo ukiendelea kufanyika.

Amemuagiza Mwenyekiti wa kamati ya mazingira kufuatilia fedha hizo na kupitia andiko la mradi huo lilikuwa linahitaji nini, kwani amebaini zipo fedha ambazo zimeidhinishwa kwa ajili ya kununua vifaa, lakini hadi sasa vifaa hivyo havijaonekana.

“Nimetengeneza timu ambayo itakuja na majibu sahihi, nitoe salamu kwamba kama kuna fedha mtu amepita nayo pembeni aanze kuirejesha mapema, tunataka matokeo makubwa ya mradi huu kuunusuru mto Katuma,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Tanganyika, Juma Shaban amesema tayari ameshatoa maelekezo kwa mkaguzi wa ndani afanye ukaguzi wa kina katika mradi huo, ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wote watakaobainika katika taarifa itakayotolewa.

“Hatuwezi kuvumiliana katika utekelezaji wa miradi, ukijaribu kufuatilia kwa kina kuna vitu unaviona haviko sawa kama alivyosema mheshimiwa DC,” amesema.

Naye Enock Mwaitebele kutoka Tume ya Maadili ya viongozi wa umma akitoa mafunzo kuhusu uwajibikaji wa pamoja ameliambia Baraza la Madiwani kuwa katika dhana ya uwajibikaji serikali haiko tayari kuona kiongozi kwa uzembe wake akisababisha wananchi waichukie Serikali yao badala yake mtumishi mzembe atachukuliwa hatua.

Habari Zifananazo

Back to top button