Usipochanja Mbwa, Paka faini Sh milioni 10 au Jela

ILI kudhibiti kuenea na  kusambaa kwa ugonjwa wa kichaa cha Mbwa  sheria inasema kila mfuga mbwa au paka kumchanja ili kuzuia kichaa cha mbwa na endapo hatozingatia basi adhabu yake ni faini ya kati ya Shilingi 500,000 hadi Shilingi milioni 10  au kifungo cha mwaka mmoja jela.

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo na Kinga Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Hezron Nonga anasema ukiamua kufuga mbwa, basi mfungie ili asizurure mtaani anakoweza kusababisha madhara na unatakiwa kumchanja.

“Kanuni ya uchanjaji wa mifugo ya mwaka 2020 inamlazimu kila mfuga mbwa au paka kumchanja ili kuzuia kichaa cha mbwa na endapo hatozingatia basi adhabu yake ni kifungo au faini au vyote kwa pamoja.” Amesema

Kauli ya Dk Nonga imekuja ikiwa ni maadhimisho ya maadhimisho ya siku ya Kichaa cha Mbwa Duniani yanayofanyika kila mwaka Septemba 28 ambapo Tanzania inaripotiwa watu 15,339 wameng’atwa na Mbwa  kati ya Januari hadi Agosti 2022  na watu 1,499 wanakadiriwa kufariki kutokana na ugonjwa huo.

Mganga Mkuu wa Seriakali Dk Aifello Sichwalwe amesema idadi hiyo imepungua kutoka matukio 39,787 yaliyorekodiwa kipindi cha  mwaka 2021.

“Takwimu hizi ni kutoka kwa watu walioripoti kwenye vituo vyote vya kutolea huduma, kuna waathirika ambao hawajifika katika vituo hivyo. Utafiti uliowahi kufanywa nchini mwaka 2002 ulikadiria vifo 1,499 husababishwa na kichaa cha mbwa,” anasema Dk Sichalwe.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonyesha kichaa cha mbwa  husababisha takriban vifo 70,000 kila mwaka.

Takwimu zinaonyesha Tanzania ina mbwa zaidi ya milioni 4.5 na asilimia 98 ni wa kienyeji ambao wanaachiwa wazurure mtaani. Mbwa hao ni wanaofugwa mjini na wale wa vijijini, hasa katika jamii za wafugaji ambazo huwatumia kuimrisha ulinzi wa mifugo.

Mkoa yenye idadi kubwa ya mbwa ni Arusha, Morogoro, Iringa, Tabora na mikoa yote ya kanda ya ziwa ambako kuna wafugaji wengi.

Dk Sichalwe anasema serikali inaendelea kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya kichaa cha mbwa kwa sababu mtu akipata ugonjwa huo ni vigumu kupona, hivyo wanajikita kuzuia badala ya kutibu.

Kwa upande wake, Dk Nonga anasema hamasa ya kuchanja mifugo hiyo imekuwa ikiongezeka kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2021/22, mbwa milioni 1.6 na paka 6,833 walichanjwa kuzuia kichaa cha mbwa.

Idadi hiyo iliongezeka kutoka mbwa 986,195 na paka 5,152. Katika mwaka huu wa fedha, anasema kati ya Julai na Septemba wameshachanja mbwa 323,638 na paka 28,933 kwenye halmashauri 101.

“Tahadhari muhimu kwa jamii kuizingatia ni kuepuka kumchokoza au kumpiga mbwa anayepita barabarani kwani anaweza kukung’ata,” anashauri Profesa Nonga.

Ingawa dunia itaadhimisha Siku ya Kichaa cha Mbwa Septemba 28, Tanzania imetangaza wiki ya kuelimisha ugonjwa huo kuanzia Septemba 26 mpaka Oktoba 2 huku serikali ikilenga kuchanja mbwa na paka 60,000.

Habari Zifananazo

Back to top button