WAZIRI wa Fedha, Mwigulu Nchemba amesema Rais Samia Suluhu Hassan ameondoa usumbufu ambao wananchi wamekuwa wakiupata kutokana na mikopo ya kausha damu kwa kumwelekeza Mkurugenzi wa Benki Kuu na Idara inayosimamia fedha kupitia upya masharti ya leseni hizo ambazo watu wanajipangia riba.
Pia amesema leseni hizo zitapitiwa upya na zinatolewa kwa masharti ambayo yatakuwa na wigo kama mabenki yanavyotoa mikopo hivyo hakutakuwa na utozaji holela wa riba kama ambavyo ilikuwa ikifanya baadhi ya Taasisi.
Mwigulu alieleza hayo Jana mkoani Singida baada ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda alipokuwa kwenye ziara yake mkoani hapo kumtaka aeleza umma juu ya kauli ya Serikali kuhusiana na malalamiko dhidi ya mikopo maarufu kama kausha damu.
“Jambo hili lilimkera Rais Samia Suluhu Hassan na kuamua hatua zichukuliwe, kama kuna jambo mahususi ambalo linaendelea iwe hapa Singida au kwingine, wananchi wafike ofisi ya Mkuu wa Mkoa hivyo wao, watafika na timu yao itafika na kuchukua hatua, ili mtu yeyote anayetaka kuchukua hatua afuate sheria na kanuni,” alisema Mwigulu.
Alisema ni kweli kulikuwepo changamoto hiyo ya baadhi ya Taasisi za kifedha zinazojiamualia kukiuka sheria za leseni ambapo riba wanayopata inakuwa niyakwao sio ya Wizara ya fedha wa wala Wizara haijawai kunufaika nazo.
“Taasisi zingine zilikuwa na riba mara asilimia 50, zingine 100 na zingine 200, sio wananchi wa kawaida tu bali wengine ni watumishi wa umma nao walikuwa katika kilimo hicho,”alisema.
Nchemba alieleza kuwa, kwasasa kuna leseni ambazo zimeshafutwa kwasababu ya kukiuka masharti ambayo hayana ubinadamu ndani yake,”
“Pili kwasababu ya unyanyasaji, ikiwemo kuwaweka mahabusu jambo ambalo ni kinyume na taratibu na wote waliokuwa wakifanya hivyo leseni zao zimefutwa,” alisema.
Katika hatua nyingine Makonda alimuagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kuhakikisha anawasimamia vyema maofisa ugani watoke mjini waende vijiji yaliko mashamba kwa ajili ya kuwasaidia wakulima.
“Bashe usipochukua hatua Chama kitakuchukulia hatua, kwani haiwezekani vifaa vya kisasa vitolewe ikiwemo vile vya usafiri alafu wakae navyo mjini tu wanastarehe,” alisema Makonda.
Alisistiza maofisa hao watoke waende mjini wakaangaike na mashamba huku akiwataka wakuu wa wilaya, Wakurugenzi na Wakuu wa Idara kuandaa mashamba darasa ya mfano kwa ajili ya kuwapa elimu wakulima.
Alisema Rais Samia amekuwa akifanya jitihada mbalimbali za kukuza kilimo na kutafuta masoko kupitia ziara zake mbalimbali anazozifanya nje ya nchi lakini kuvutia mikutano mikubwa ya kimataifa ya kilimo na chakula kufanyika hapa nchini hivyo wanakila sababu ya kuendeleza jitihada hizo.
“Mlimuona Rais Samia akiwa China, akiwaomba soko la mazao ya mihogo ambayo yamevunja rekodi kwenda huko, alienda India akapata soko la Mbaazi, Chokolo, Maharage yote hiyo inamaanisha soko la uhakika lipo,” alisema.
Aliongeza kuwa Rais Samia ameboresha na kuweka mifumo ya umwagiliaji na mwaka 2024 ametoa zaidi ya sh bilioni 500 kati ya hizo bilioni 300 zinakwenda katika ruzuku ya mbolea.
“Rais Samia anaangaika na mbegu bora anataka Taifa hili lijitegemee kiuchumi, hivyo kama wataalam wa kilimo wakiachwa bila kwenda vijijini kuwasaidia wakulima hawatopiga hatua,” alisema.
Alisema Rais Samia ameweka nguvu kubwa katika Kilimo kama ambavyo Mwalimu Julius Nyerere aliwekeza katika miradi mbalimbali ikiwemo ule wa Building Better Tomorrow (BBT).
“Rais Samia ametoa fedha nyingi kwenye kilimo, amewapa maofisa ugani pikipiki na kompyuta mpakato na wote wamepewa vifaa vya kupima rutuba ya udongo na vifaa vya maji nchi nzima cha hajabu na kushangaza wako mjini,” alisema.
Pia alimuagiza Waziri Bashe kuhakikisha maofisa hao wanaandaa ripoti ya hali ya kilimo katika vijiji vyao na namna walivyo wahudumia wakulima.
Aidha aliwaagiza Wakurugenzi kutoa mafuta kwa maofisa hao ili wawafikie wakulima kwa wakati na yeyote anayeweka kizuizi katika hilo, atachukuliwa hatua na Waziri husika.
“Chama kinaelewa kuwa siasa na uchumi ni kilimo, kama ambavyo kanuni na miongozo mbalimbali ya Chama inaeleza hivyo hatutafanya mchezo katika kusimamia maendeleo ya sekta hiyo na kukuza uchumi kwa wananchi,” alisema.