Usyk bingwa asiyeshindika, amduwaza Fury

RIYADH, Saudi Arabia: BONDIA wa Kiukreni, Oleksandr Usyk amemshinda Tyson Fury, bondia wa Kiingereza, kwa tofauti ya alama na kuwa bingwa wa uzito wa juu asiye na mpinzani ‘the undisputed’ kwa kutwaa mikanda yote ya uzito wa juu inayotambulika kimataifa.
Katika Jiji la Riyadh, Uwanja wa Kingdom Arena nchini Saudi Arabia, usiku wa kuamkia leo Usyk amevunja historia iliyodumu kwa takribani miaka 24 tangu Lennox Lewis aliposhikilia heshima hiyo kwa miezi mitano mnamo 1999 na 2000.
Usyk mwenye mikanda ya WBA, IBF na IBO ameongeza kabatini taji la WBC lililokuwa likatwaliwa na Fury kwa kushinda pambano kwa namna ya kipekee.
Pambano hili lilikuwa la kusisimua, huku likiwa na mabadiliko ya uongozi kati ya mabingwa wawili wa uzito wa juu ambao hawajawahi kushindwa hapo awali. Katika raundi ya tisa, Usyk alifanikiwa kumuangusha Fury, na kuimarisha nafasi yake ya kushinda.
Matokeo ya Majaji wawili yalimpa Usyk ushindi wa alama 115-112 na 114-113, wakati Jaji wa tatu akimpa Fury ushindi kwa alama 114-113.
“Ni wakati mzuri. Ni siku kubwa,” amesema Usyk kwa furaha baada ya ushindi wake.
Usyk, aliyekuwa bingwa wa uzito wa cruiserweight, alipanda uzito wa juu na haraka akapata umaarufu kwa ushindi wake dhidi ya mabingwa wengine. Pambano hili lilikuwa moja wapo ya yaliyosubiriwa kwa hamu kubwa, likikusanya mashabiki wengi kutoka kote ulimwenguni.
Tyson Fury, anayejulikana kwa mbinu zake za kipekee na uwezo wake wa kushinda wapinzani wenye nguvu, aliingia kwenye pambano hili akiwa na rekodi bora. Hata hivyo, Usyk alionesha ustadi wa hali ya juu na mbinu bora, ambazo zilimpa ushindi kwa uamuzi wa mgawanyiko wa majaji.
Kwa ushindi huu, Usyk amejijengea historia katika ndondi kwa kuwa bingwa wa kwanza wa uzito wa juu asiye na mpinzani kwa zaidi ya miaka 20, tangu enzi za Lennox Lewis.
Ushindi huu unamfanya Usyk kuwa mmoja wa mabingwa wakubwa zaidi wa ndondi katika kizazi chake.

Habari Zifananazo

Back to top button