Utafiti: Asilimia 85 wanafunzi hawashirikishwi vikao

ASILIMIA 44.4  ya wanafunzi wa Sekondari hawaelewi maana ya demokrasia, huku asilimia 85.5 hawajawahi kushiriki, kushirikishwa katika vikao rasmi vya shule vinavyofanya uamuzi.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 22 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu HakiElimu, Godfrey Boniventure katika hafla ya uzinduzi wa ripoti ya utafiti wa Mchango wa Elimu ya Uraia Shule za Sekondari na ushiriki wa vijana katika michakato ya kidemokrasia nchini.

Amesema utafiti huo umebaini kuwa asilimia 68.9 ya wanafunzi hawajawahi kugombea au kuonesha nia ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi ngazi ya shule, huku asilimia 44 hawashiriki katika chaguzi za uongozi wa wanafunzi.

“Asilimia 26 hawajawahi kushiriki kabisa katika midahalo na mijadala ya hoja kama sehemu ya kuwajengea uwezo wa ushawishi na demokrasia,”amesema Boniventure.

Amesema utafiti huo, uliofanyika katika Wilaya za Mkuranga, Tabora, Ukerewe, Kilwa, Sumbawanga  na  Arusha, unaonesha ushiriki hafifu wa vijana katika mifumo ya kidemokrasia ndani na nje ya shule unachangiwa na upungufu katika mtaala wa elimu ya uraia itolewayo shule za sekondari.

Pia utafiti umebaini kuwepo kwa changamoto kubwa katika mtaala wa somo la uraia shule za sekondari, ambao kwa kiwango kikubwa haumpi mafunzo stahiki mwanafunzi yatakayomfanya aelewe vyema na kushiriki shughuli za kidemokrasia katika ngazi mbalimbali kwa nafasi yake.

Kwa upande wa walimu utafiti huo umebaini kuwa sehemu kubwa ya walimu ambao wanafundisha somo la uraia, hawana maarifa stahiki yanayowawezesha kuwafundisha na kuwaaandaa vijana kuelewa maana ya siasa safi.

Naye Perpetua Almasi ambaye ameshiriki katika utafiti huo akiuelezea zaidi, amesema asilimia 47 ya viongozi wa wanafunzi shule za sekondari hawapatikani kwa njia ya chaguzi za demokrasia.

 

Kamishna wa Elimu Tanzania Dk. Lyabwene Mtahabwa, akiwa na baadhi ya wanafunzi wa shule za sekondari, akizindua ripoti ya utafiti wa Mchango wa Elimu ya Uraia Shule za Sekondari na Ushiriki wa Vijana katika Michakato ya Kidemokrasia nchini.

“Utafiti umeonesha walimu wanawachagulia wanafunzi viongozi,  unakuta yule anayeonekana kuwa na uwezo wa masomo ndio anapewa nafasi ya uongozi, hata kama hana sifa za uongozi, na kuna mwingine hana uwezo sana wa darasani ,lakini ana uwezo wa uongozi ananyimwa fursa wa kigezo cha kutokuwa na uwezo hii si sawa,” amesema Perpetua.

Amesema asilimia 11 ya wanafunzi wanajitolea katika uongozi na asilimia 42 ndio wanapatikana kwa kufanyika kwa chaguzi.

Amesema katika ngazi ya jamii asilimia 80 ya vijana walioko shuleni hawajawahi na hawahamasishwi kushiriki mikutano ya kampeni za siasa, asilimia 67.8 hawajawahi kuhudhuria mikutano ya kijiji au mitaa na asilimia 67.5 hawajawahi kuona umuhimu wa wao kushiriki shughuli za kijamii.

Perpetua akitoa maependezo ya tafiti hiyo wameitaka serikali kupunguza umri wa vijana kupiga kura hadi kufikia miaka 14 badala ya 18, ili kutoa fursa kwa vijana kuanza kushiriki mchakato wa siasa na demokrasia mapema zaidi na kujenga uwezo na maarifa ya uongozi na kidemokrasia.

Naye Kamishna wa Elimu nchini, Dk. Lyabwene Mtahabwa, amesema ameupitia utafiti huo una mapendekezo mazuri, ambayo watayafanyia kazi kwa kuyaingiza mapendekezo hayo katika maboresho ya mitaala yanayoendelea.

“Ujenzi wa moyo wa demokrasia utakua na manufaa kwa watoto kama watajengewa uzalendo, demokrasia isiyo na uzalendo inatia shaka, demokrasia inanawiri, inakuwa baraka kama imekuwa kwenye moyo wa uzalendo,” amesema.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x