Utafiti uzalishaji miche maabara unavyoongeza thamani ya mazao

UTAFITI wa miche bora ya mimea ni sehemu muhimu katika kupata mazao bora na yenye tija kwa mkulima, ili kuweza kunufaika na kilimo.

Katika Kufanikisha hilo Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania(TARI)  inafanya tafiti mbalimbali, ili waweze kuwasaidia wakulima kulima kilimo chenye manufaa zaidi.

Kituo chao cha TARI-Mikocheni ni moja kati ya vituo 17 vinavyofanya utafiti wa kilimo, ambapo pamoja na mazao mengine lakini wao pia wamejikita zaidi katika kuendeleza zao la minazi na kusimamia masuala yote ya bioteknolojia.

Advertisement

Mratibu  wa Uhaulishaji Teknolojia na Mahusiano wa TARI, Kituo Cha Mikocheni jijini Dar es Salaam, Vidah Mahava anasema kuwa taasisi hiyo  imekuwa ikijikita kufanya utafiti katika mazao mbalimbali ya chakula na biashara, ili kujua mbegu bora na namna nzuri ya kilimo .

Anasema wamekuwa wakitumia teknolojia ya chupa(Tissue Culture), kuzalisha miche na  miongoni mwa mazao wanayofanyia utafiti hivi sasa ni nanasi, mkonge, mihogo, minazi , viazi vitamu na mazao mengine.

Mtafiti wa TARI Christina Kidulile akionesha mbegu za nanasi zilizotolewa maabara

Mahava anasema pia wamekuwa wakiwaambia wadau wa mazao ya kilimo  kufuata kanuni bora za kilimo na kutumia miche yao ambayo wameifanyia utafiti na kuipatia huduma bora ili iweze kuzaa zaidi.

MKONGE KUZALISHWA KWA CHUPA

Kituo cha TARI-Mikocheni  kimeanza kuzalisha  miche 500,000 ya zao la mkonge hadi kufikia Julai, 2023 kwa kutumia teknolojia ya chupa,  ili kutoa miche bora na kwa ajili ya uzalishaji.

Mtafiti kutoka TARI-Mikocheni, Margareth Lupembe anasema mbegu hizo zote zinazalishwa kwa njia ya chupa ndani ya maabara.

Lupembe anasema pia wanaendelea na uzalishaji wa miche bora ya zao la nanasi, ambalo hukaa muda mrefu bila kuharibika na lenye ubora wa kuuzwa nje ya nchi bila tatizo.

Anabainisha kuwa  wamekuwa wakitumia teknolojia hiyo ya chupa maarufu kama Tissue Culture kwa muda mrefu, ambapo mmea huzalishwa ndani ya chupa iliyokuwa na virutubisho vyote vinavyosaidia mmea kukua kama unavyokuwa nje.

Mtafiti wa TARI Christina Kidulile akionesha mbegu za nanasi zilizotolewa maabara

“Tunatakiwa  kuzalisha miche ya Mkonge 500,000, ifikapo Julai mwaka huu kwa ufadhili wa serikali kupitia TARI Mlingano, ili iweze kusambazwa kwa wakulima, pia kuna mazao mengine kama migomba, mihogo na viazi vitamu ambayo yote tunazalisha kwa kutumia teknolojia ya chupa.”anasema Lupembe.

Lupembe anafafanua kuwa uzalishaji wa mbegu bora kwa njia ya chupa ni tofauti na uzalishaji wa mbegu kwa njia zingine kama GMO, hivyo ni muhimu wakulima na wadau wengine wa kilimo kujua hilo.

“Faida ya uzalishaji huu ni inatunza vinasaba, mimea yote inafanana kwa kuwa itatoka katika shina moja, lakini pia ladha ni ile ile na mbegu zake zinaweza kupandwa kama kawaida, nyingine ni kupunguza mahitaji ya uhaba wa mbegu kwa kuwa mbegu moja inatoa miche mingi,” anasema.

ZAO LA NAZI KUZALISHWA PIA

Mahava anasema TARI-Mikocheni  ndicho kituo pekee kinachosimamia zao la minazi na malengo yao ni kuhakikisha kuwa linachangia pato la taifa na mazao ya mafuta.

“Kwa sasa nazi tunazozigawa zina uwezo wa kuzaa nazi 35 mpaka 45, ambapo utafiti unataka kufika mpaka nazi 70, hivyo kuna mbegu ambazo wamekuwa wakizigawa kwa wadau wao,” anasema.

Anaeleza kuwa mikakati mikubwa ambayo wanaifanya ni kuhakikisha wanaweza kufanya kazi na wadau mbalimbali, ili kufufua zao la minazi kwa kutumia kanuni bora za kilimo.

Mtafiti Magreth Lupembe akiwa katika mainesho na mananasi na miche ya mananasi jijini Dar es Salaam

” TARI inafanya utafiti wa mazao kwa kuvumbua mbegu kwa kutatua matatizo ya wakulima nchini, ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mazao yao hususani wadudu,” anasema.

Anasema kwa sasa nazi ina mahitaji mengi na zinahitajika sana kutokana na matumizi yake, hivyo bado hatujaweza kukidhi mahitaji hayo.

“Naomba niwaambie kwamba hata nazi mnazoziona watu wanazozipikia  bado mahitaji ni makubwa na zile zinazotumika viwandani nyingine zinaagizwa kutoka nje ya nchi,”anasema Mahava na kuongeza:

“Minazi inaanza kuzaa kuanzia miaka mitano hadi saba na hii ndio minazi tuliyonayo, lakini hapa katikati iliwahi kuletwa minazi inayoanza kuzaa miaka mitatu ni sawa, lakini bado ilionekana haifanyi vizuri sana na inaonekana ikizaa baada ya muda mfupi inakufa kutokana na magonjwa, lakini pia haikuweza kustahimili hali ya hewa,” anasema.

Anaeleza kuwa minazi ambayo wamefanyia utafiti na ambayo wanasambaza sasa ni minazi ya asili inayoitwa East African Tall, ambayo inaanza kuzaa baada ya miaka mitano hadi saba na inaweza kuzaa hadi nazi 70 na kuendelea, lakini pia wanaendelea kufanyia utafiti zaidi ili iweze kuzaa nazi nyingi zaidi zinazofikia 100 na kuendelea.

“Minazi mingi iliyopo ni ile ambayo wamepanda siku nyingi sana hivyo kauli  yetu mara nyingi tumekuwa tukiwaambia wadau kwamba sasa waanze kupanda minazi mipya na ile iliyopo wailime kwa kufuata kanuni bora za kilimo, lakini pia mingi iliyopo ukiangalia kwa haraka haihudumiwi,”anabainisha Mahava.

Ameendelea kusema kuwa mikakati mikubwa ambayo wanaifanya ni kuhakikisha wanaweza kufanya kazi na wadau mbalimbali, ili kufufua zao la minazi kwa kutumia kanuni bora za kilimo.

UELEWA MDOGO CHANGAMOTO

Mahava anasema kumekuwa na changamoto kwa jamii kutokujua kuhusiana na kituo hicho kufanya uzalishaji wa mbegu kwa njia ya chupa.

‘Watu wengi wanakuwa na taarifa tofauti wengine wanafikiria kwamba tukienda Mikocheni kuwa ni GMO wanaiweka bioteknolojia na GMO kumbe yote hayo yanatokana na wananchi kutokuwa na taarifa kamili kuhusiana na kituo hiki na utafiti wetu unavyofanya kazi,”alisema Mahava.

Mbegu zilizohifadhiwa katika maabara TARI Mikocheni

TUNALENGA KUTATUA CHANGAMOTO

Mtafiti Chona Mahushi anasema lengo la utafiti ni kutatua changamoto za masuala ya kilimo kwa wakulima hivyo minazi mirefu ambayo wao ndio wanayoifanyia utafiti ndio bora zaidi kwa kuwa inakaa muda mrefu na inahimili magonjwa mbalimbali.

Anasema wakulima wa zao hilo na wengine wameombwa kufika katika vituo hivyo vya utafiti vilivyo katika kila eneo nchini, ili waweze kupata ufumbuzi wa matatizo yao ya kilimo kulingana na mazao wanayozalisha, ili wafaidike na kilimo chao.

Anaeleza kuwa kilimo cha minazi sasa kimeanza kuonekana kama ni fursa zaidi, ambapo faida zake ni pamoja kuzalisha mbao ambazo zinatengeneza vitu mbalimbali, ikiwemo samani za ofisini, nyumbani na hata wakati mwingine kutumika kama mihimili ya madaraja ya asili, kuzalisha nazi zinazotumika kama kiungo katika mboga, mafuta ambayo watu hujipaka mwilimi, ufagio maarufu kama fagio la chelewa.

MIPANGO KUWAFIKIA WANANCHI

Mahava anasema kituo cha utafiti kimepanga mikakati yao katika utafiti wanaoufanya kwa sasa ni kuwa na mbegu ambazo zinakinzana na magonjwa, ukame na zinazaa kwa wingi.

Pia inaelezwa kuwa  mikakati yao ni pamoja na kushirikiana na Halmashauri mbalimbali nchini na wadau katika kugawa mbegu ambazo zimefanyiwa utafiti kwenye mikoa ambayo inalima nazi nchini, ili waweze kustawisha vitalu vyao katika zao la minazi.

Anasisitiza kuwa TARI inafanya utafiti wa mazao kwa kuvumbua mbegu kwa kutatua matatizo ya wakulima nchini, ambayo yamekuwa yakitokea kwenye mazao yao hususani wadudu.

Naye mtafiti  kwa upande wa maabara ya Tissue Culture , Christina Kidulile anasema katika maabara hiyo wanazalisha mimea na wamekuwa wakitumia vifaa mbalimbali vinavyosaidia mimea kuota.