WATUMISHI wa afya kutoa lugha zisizofaa ni baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwenye utafiti uliofanywa kwa sekta ya afya wilayani Mlele.
Utafiti huo umefanywa na taasisi isiyo ya kiserikali iitwayo Usevya Development Society (UDESO), kupitia Kamati ya ufuatiliaji matumizi ya rasilimali za Umma (PETS).
Akisoma matokeo ya ripoti hiyo kwa mgeni rasmi, ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, Majid Mwanga, Katibu wa Kamati ya PETS, Emida Kimisha, amesema licha ya mazuri ya watumishi katika sekta ya afya, lakini bado zipo changamoto za baadhi ya watumishi kuchelewa kuwapatia huduma wagonjwa, jambo linalosababisha kukimbilia vituo binafsi.
Amesema utafiti walioufanya wamebaini bado mazingira ya kutolea huduma katika zahanati na vituo mbalimbali vya afya si rafiki, ikiwemo upungufu wa vitendea kazi katika zahanati ya Mbede, ukosefu wa uzio Zahanati ya Mbede na Kibaoni, hali inayosababisha watoto kuingia kirahisi kuokota makopo ya dawa na mifugo kukatiza.
“Kuna mifumo isiyo rafiki ya utunzaji wa nyaraka za taarifa muhimu kama vile nyaraka fedha, mihutasari ya vikao, kumbukumbu za matumizi na namna ya makabidhiano ya majukumu katika Zahanati ya Kibaoni na Kituo cha afya Usevya.
“Uhusiano hafifu kati ya idara ya afya na idara zingine katika ngazi ya halmashauri kiasi kwamba uratibu wa taarifa zilizokuwa zinahitajika hazikutolewa, ili kamati ya PETS waweze kuzitumia katika uchambuzi wa taarifa,”amesema.
Baada ya kupokea taarifa hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Majid Mwanga ameipongeza taasisi ya UDESO kwa kutoa ripoti hiyo kwa kile alichodai itaisaidia serikali kujua wapi kuna changamoto na kufanyia kazi yote yaliyobainishwa, ili kuongeza ufanisi zaidi.
Ameitaka taasisi hiyo kujikita zaidi kuibua na kuisaidia jamii dhidi ya ukatili wa kijinsia na maadili kwa kuwa ni moja ya vitendo vinavyozorotesha ustawi wa jamii.