Utafiti wahitajika ulipaji pensheni kwa wazee wote

NAIBU Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Patrobas Katambi amesema utafiti wa kina unahitajika kufanyika ili kuona uwezo wa Serikali katika kulipa pensheni kwa wazee wote.

Katambi ametoa maelezo hayo Bungeni Dodoma leo Jumatano wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Hawa Mchafu Chakoma aliyetaka kufahamu hatua iliyofikiwa na Serikali katika mchakato wa pensheni kwa wazee wote.

“Mheshimiwa Spika, Pensheni kwa wazee wote inajumuisha wazee ambao walikuwa katika ajira ambao kwa sasa wanalipwa pensheni na Mifuko waliyochangia wakati wanafanya kazi na pili wazee ambao hawajawahi kuajiriwa kwa sasa hawalipwi,” Katambi ameliambia Bunge.

Advertisement

Hata hivyo, Naibu Waziri amefafanua katika jibu lake kuwa mchakato wa kuwalipa pensheni wazee wote ambapo utajumuisha wazee ambao hawajawahi kuajiriwa ni utaratibu mpya ambao utahitaji kugharamiwa na bajeti ya Serikali.

Ameongeza kuwa kwa sasa Serikali imekuwa inahudumia wazee kutoka katika familia au kaya zenye umaskini uliokithiri kupitia mradi wa Kunusuru Kaya Maskini (TASAF) ambapo wazee ni sehemu ya familia hizo.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *